
HAPA kwenye Love & Life ni mahali sahihi pa kuongeza ufahamu kuhusu mambo ya uhusiano na mapenzi. Naamini kila siku umeendelea kuelimika kupitia hapa.
Yes! Leo nitazungumzia juu ya kuweza kuushinda upweke katika moyo wako. Natambua kuna baadhi ya wanawake au wanaume wanakaa kipindi kirefu bila ya kutamkiwa kuwa wanapendwa, kutokana na hali hiyo wanakuwa wapweke na wakati mwingine kufikiria kuwa wao ni wabaya na wasiostahili kabisa kuwa na wapenzi.
Wengine huanza kujiona hawafai kutokana na sababu ambazo wenyewe wataziweka ambazo kwa kiasi kikubwa huwa za kujikosoa.
Wakati mwingine utakuta mwanamke anaanza kufikiria kuwa huenda kwa sababu yupo katika hali fulani ndiyo maana hapati mtu wa kumpenda na fikra nyingine mbaya juu yake ambazo huwa ni za kujikatisha tamaa.
Tambua kitu kimoja; kuna wasichana warembo na wavulana watanashati wengi ambao hawajapata pumziko la kweli katika mioyo yao kwa muda mrefu sasa, wamekuwa wakitafuta watu wenye mapenzi ya kweli kwa muda mrefu bila mafanikio na sasa wamekata tamaa ya kupata wapenzi wa kweli na badala yake wamegeuka vyombo vya starehe.
Wavulana watanashati au wasichana warembo mara nyingi watu wa upande wa pili huwatamani zaidi kuliko kuwa na mapenzi ya kweli, kwa maana hiyo baada ya kushiriki naye ngono mara kadhaa huamua kuachana naye na kumuacha muhusika akiwa na sononeko katika moyo wake.
Watu wa aina hii huachwa na dhiki ya moyo na wakati mwingine hukata tamaa na kuamua kutokuwa na uhusiano mwingine kabisa na wapenzi wapya. Jaribu kufikiri kama kuna mtu wa aina hii ambaye amekuwa akitoneshwa mara kadhaa na wapenzi na wewe ambaye una miezi karibu sita sasa hujapata akupendaye nani mwenye matatizo zaidi? Nadhani jibu yakinifu utakuwa nalo.
Inawezekana wewe ni mmoja kati ya hao ambao wana sononeko la moyo kwa kutopata faraja ya kweli kwa wapenzi wao.
Hakika hizi ni mada mbili tofauti lakini leo nitaanza na hili la kutopata mpenzi kwa muda mrefu na sasa umekata tamaa ya kupendwa, kuoa au kuolewa katika siku zote za maisha yako.
Wakati mwingine inawezekana hujafahamu chanzo cha kutopata mpenzi, lakini kuna mambo mengi ya kuzingatia ili uweze kupata mpenzi na hivyo kuepuka upweke katika moyo wako.
ANZA KWAKO KWANZA
Jichunguze kwanza wewe. Jiulize, unajijali? Inawezekana ukawa na maswali lukuki kutokana na ninavyouliza, unajijali! Nataka utambue kitu kimoja, kuwa kuna baadhi ya watu hawajipendi! Hivi unadhani kama wewe mwenyewe hujipendi, hujithamini nani atakupenda?
Ninaposema ujipende namaanisha ujipe upendo ule wa kawaida wewe mwenyewe kabla ya kuhitaji upendo wa mtu mwingine.
Mwingine anaweza akawa anavaa nguo chafu, hapigi pasi, nywele zipo timtim, kifupi yupo hovyohovyo, sasa nani atampenda mtu wa staili hiyo?
Hebu tukomee hapa kwa leo, ukibaki na msingi mmoja wa kujipenda kwanza, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
No comments:
Post a Comment