Dk. Reginald Mengi.
Hii ni sehemu ya pili ya makala yetu ya ujasiriamali, kama tulivyoanza nayo wiki iliyopita, nikisisitiza kuwa siku zote utajiri huanzia mawazoni badala ya kuwa mdomoni kama wengi wetu tunavyokuwa.
Watu wengi hufikiri kuwa ili waweze kuwa na hali nzuri kifedha, ni lazima kwanza wawe na fedha. Hii si kweli, unaweza kufikiria na hatimaye kuwa na mamilioni ya shilingi ukianzia na sifuri kabisa, kama wengi wetu walivyoweza kufanikiwa.
Kitu cha msingi ni kuelewa unataka kuwa nani, kwa jinsi gani na kadhalika. Hatua ya kwanza ya kutengeneza fedha bila kuwa na mtaji ni kujielewa wewe mwenyewe na kutambua malengo yako, maana wapo watu ambao hawajitambui na wala hawajui wanataka kuwa vipi hapo baadaye.
Baada ya hapo ni lazima pia kutambua uhalisi wa malengo yako, maana baadhi ya watu huweka malengo makubwa yasiyotekelezeka, kwa hiyo kama kutakuwa na maswali ya kujiuliza, fanya hivyo na kisha endelea mbele, hakikisha kila siku inayokwenda, inakuwa na kitu chako cha kujivunia. Kukaa na mawazo mazuri na kuyafungia kabatini ni sawa na kupoteza muda.
Malengo hayawezi kutimia kama ndoto, unatakiwa kuwa na mipango na utekelezaji wake. Wakati unapojiandaa kutimiza malengo yako, ni lazima pia kujifunza namna ya kupunguza gharama za matumizi yako.
Kama ulikuwa unatumia gari kwenda na kurudi kazini kwako, huu ni wakati muafaka sasa wa kulipaki gari lako na kuanza kutumia usafiri wa umma, kwa maana ya daladala.
Malengo yetu ni lazima yaanze na kuhifadhi fedha, kwa sababu tunajua inachukua muda kutengeneza fedha, kwa hiyo tunapaswa kuzingatia uadilifu mkubwa wakati tunapoanza zoezi la kujiwekea fedha kila siku.
Katika kupunguza gharama za matumizi yetu, wakati mwingine hata tunapotaka kula chakula, inabidi tukifikiri mara mbili, je, ni sahihi kula chakula cha bei mbaya? Hili ni la kuzingatia sana, hata kama akaunti yako ya benki itakuwa na fedha nyingi.
Hizi ni hatua nyepesi za kufuata ambazo baadaye zitakupa matokeo ya kushangaza, kila mara zoezi lako kubwa liwe ni jinsi gani ya kutengeneza fedha zaidi. Kutunza fedha zako kila mwezi kutaongeza kipato chako kwa vile shilingi laki moja utakayohifadhi mwezi huu, itakuwa hela nyingi baada ya miezi sita.
Na kama una watoto wanaosoma, shirikiana nao kuhakikisha nao wanatoa mchango katika uwekezaji unaotaraji kuufanya, kama vile kutowapa fedha kwa ajili ya kujinunulia chakula huko shuleni, bali hakikisha wanakula nyumbani na hivyo kuisaidia familia katika kubana matumizi.
Katika kusaka utajiri, daima watafutaji huwa hawachoki, kila siku wanataka kuona fedha walizonazo zinaongezeka, ndiyo maana hutumia vipato vyao kuanzisha vyanzo vingine vya mapato.
Watu wengi wanaamini sana katika uwekezaji.
Kama utaanzisha leo mradi wako, bila shaka baada ya miezi kadhaa uwekezaji wako utaanza kutoa matunda yanayokufanya ujiongezee malengo zaidi ya kufanikiwa. Mradi wa mwaka mmoja unaoendeshwa vizuri, unatoa mwanga mkubwa wa kuwekeza mamilioni katika miaka michache baadaye. Mfanyabiashara maarufu, mzee Reginald Mengi huwa anasema tumia kidogo kuliko unachoingiza, utafanikiwa.
GREDIT:GPL

No comments:
Post a Comment