ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 4, 2014

Utapeli:Takukuru wawadaka polisi, mfanyabiashara

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.

Askari Polisi wawili wametiwa mbaroni katika matukio mawili tofauti, likiwamo la kutaka kumtapeli mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Sh. milioni 50 wakijifanya ni maofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru).

Katika tukio la kwanza, mtu anayedaiwa kuwa askari polisi Isidory Anslem (30) mwenye namba F 8934 wa kituo cha polisi Mabatini Kijitonyama, Dar es Salaam akiwa na mfanyabiashara Kaskila Clarence (40), wakazi wa Sinza, Dar es Salaam walikamatwa juzi na askari wa bandari wakitaka kufanya utaperi bandarini.

Watuhumiwa hao baada ya kupekuliwa walikutwa na barua ya Takukuru inayodaiwa kuwa ya kughushi na bastola ambayo ilikuwa na risasi nane.

Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo unafanywa kwa ushirikiano kati ya taasisi hiyo na askari wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema amepata taarifa za tukio hilo na kwamba wenye mamlaka ya kuzungumzia zaidi suala hilo ni polisi wa Kikosi cha Wanamaji.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Wanamaji, Mboje Kange, alipoulizwa alisema alikuwa katika kikao na kuahidi apigiwe simu baadaye, lakini hadi tunakwenda mitamboni simu yake ilikuwa imefungwa.

“Mimi nipo likizo, suala hilo nimesikia, ila Polisi Marine ndio wanaoweza kuzungumzia zaidi tukio hilo,” alisema Kamanda Wambura.

Maofisa wa TPA wakizungumza na NIPASHE katika eneo la tukio, walisema watuhumiwa hao walifika bandarini wakiwa katika gari namba T 799 CHH aina ya Toyota ambayo ni mali ya askari huyo mtuhumiwa Anslem.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa watuhumiwa hao baada ya kufika bandarini hapo walionyesha barua ya hati ya wito kutoka Takukuru yenye kumbukumbu namba PCCB/IAK/01/2014 ya Juni 2, mwaka huu.

Barua hiyo ambayo baadaye iligundulika kuwa ni ya kughushi, ilikuwa na maelezo ya kumtaka mfanyakazi wa TPA, Issa Ally Kiangio, kufika Takukuru katika ofisi zilizopo Upanga mtaa wa Urambo/Kalenga saa 3:00 asubuhi Juni 3, mwaka huu.

“Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 na vifungu 10(2) na 2A vya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 vikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 8(1) cha sheria Na.11/2007, fahamu kwamba ofisi yetu inafanya uchunguzi wa mambo ambayo inaaminika kuwa una ufahamu nayo,” imeeleza barua hiyo ambayo NIPASHE iliiona.

Barua hiyo imeendelea kueleza kuwa: “Hivyo basi unatakiwa kufika katika ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyopo Upanga mtaa wa Urambo/Kalenga saa 3:00 asubuhi tarehe 03 mwezi Juni mwaka 2014.”

Barua hiyo iliyosainiwa na mtu aliyejitambusha kwa jina la E. Makale kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, imemwagiza mfanyakazi huyo wa TPA kutekeleza wito huo kama alivyoagizwa bila kukosa na kwamba kushindwa kufika ni kosa la jinai na anaweza kushtakiwa mahakamani.

Kiangio alisema kuwa baada ya watu hao kumpatia hati hiyo, walimweleza kuwa kama anataka mambo hayo yaishe asiende Takukuru awape Sh. milioni 50.

Katika tukio hilo, mtuhumiwa Kaskila Clarence ambaye alijifanya ni ofisa wa Takukuru baada ya kupekuliwa alikutwa na bastola yenye namba 306868 aina ya Browing ikiwa na risasi nane.

Kufuatia tukio hilo watuhumiwa hao wamefunguliwa jalada la upelelezi namba MUB/RB/202/2014 katika kituo cha Polisi Wanamaji.

Katika mahojiano na askari wa Bandari, watuhumiwa hao walisema wao siyo wafanyakazi wa Takukuru bali walikuwa katika harakati za kujitafutia pesa.

POLISI FEKI MBARONI IRINGA
Katika tukio la pili, Jeshi la Polisi mkoani Iringa linawashikilia watu wawili akiwamo mtu anayesadikika kuwa ni askari polisi akiwa na mwenzake anayedaiwa kuwa ni bosi wake kwa wakitaka kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi eneo la Ipogoro, Manispaa ya Iringa.

Alimtaja askari feki aliyekamatwa kuwa ni Bashir Nyalunga (20), mkazi wa Ilula ambaye alikuwa na mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Godlack Mbeale (21), mkazi wa Kihesa Sokoni

Kamanda Mungi alisema watuhumiwa hao walikuwa wakiwatapeli wananchi kwa kuwatoza Sh. 400,000 hadi Sh. 500,000 kwa madai kuwa watawatafutia kazi watoto wao.

Alisema watuhumiwa hao wakati wakitekeleza utapeli huo, mmoja wao alikuwa amevalia sare za Jeshi la Polisi na mwingine aliyejifanya bosi wake akiwa amevaa nguo za kiraia.

Kamanda Mungi alisema kuwa uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba sare zilizokuwa zikitumika katika utapeli huo ziliibwa kwa askari mmoja na kwamba upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: