MKALI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba ‘Alikiba’, anatarajia kulitumia Tamasha la Matumaini 2014 kuzindua rasmi nyimbo zake mbili zinazotikisa anga la Bongo Flava kwa sasa za ‘Mwana’ na ‘Kimasomaso’, huku akikiri kufarahishwa na mapokezi ya singo hizo kwa mashabiki nchini.
Tasnia ya muziki huo nchini kwa sasa imegubikwa na gumzo la kazi hizo mbili za Alikiba, , alizofanyia katika studio mbili tofauti za Combination Sound chini ya mtayarishaji mahiri Man Walter na MJ Records chini ya Marco Chali.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, Alikiba alisema kuwa Tamasha la Matumaini lina maana kubwa kwake na kila Mtanzania, hivyo ameamua kulitumia kuzindulia nyimbo hizo, zilizomrejesha kwa kasi baada ya kimya kirefu kilichotokana na harakati tofauti.
“Tamasha la Matumaini, kama jina lake lilivyo ni maalum kurejesha matumamini kwa waliopoteza. Niliwahi kupoteza matumaini ya harakati zangu huko nyuma wakati naanza tasnia hii, lakini kupitia kitu kama hiki, nikaweza kusimama na kuwa Alikiba mwenye jina na mafanikio niliyonayo sasa,” alisema mkali huyo.
Aliongeza kuwa kwa kutambua hilo amewataka Watanzania kumiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa Agosti 8, kushuhudia shoo kali atakayofanya sanjari na nyota wengine wa muziki huo watakaotumbuiza katika tamasha hilo, ambalo litawarejeshea matumaini katika nyanja na tasnia tofauti walizomo.
Alisema baada ya tamasha, ataanza rasmi mchakato wa kuandaa video ya vibao hivyo, alivyovitaja kuwa ni zawadi maalum kwa mashabiki wake, ambao walimpa wakati mgumu akitafakari namna ya kutii kiu.
“Kimya kingi kina mshindo mkuu kaka. Nilibanwa na masuala mbalimbali, kama vile michakato ya kibiashara, mapumziko maalum yaliyotokana na kufululiza muziki kwa muda mrefu na pia kumpaisha bwana mdogo (Abdul Kiba). Sasa niko kamili, hakuna kulala wala kupumzika tena, ni ‘non-stop’ kwa kwenda mbele,” alisema Alikiba.
CREDIT:MTANZANIADAIMA
No comments:
Post a Comment