ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 31, 2014

SIMULIZI TAMU YA BAHATI BUKUKU -8

ILIPOISHIA:
KATIKA kila neno nililokuwa nikiongea mahali hapo nilikuwa nikijiamini. Msichana yule akaanza kuniangalia kuanzia juu mpaka chini, akayarudisha macho yake chini mpaka juu, akakunja uso wake kwa hasira. Nikaona siku ile lingetokea balaa mahali pale.
ENDELEA NAYO....YESU AMBADILISHA MAISHA
Huo ndiyo ulikuwa mwaka wangu wa mwisho kuwepo pale shuleni, katika maisha yangu yote kipindi hicho nilikuwa nikimtumikia Mungu, kila siku wanafunzi walitakiwa kuiga mfano wangu kwani maisha yangu yalikuwa ni ya kawaida sana.
Sikuwa na maringo, sikuwa mgomvi, kwa sababu Yesu alikuwa akiishi ndani yangu, maisha yangu yalikuwa ni ya kitakatifu sana.

ASHUSHA MAHUBIRI
Katika kipindi cha mwishomwisho kabisa, niliwahubiria wanafunzi wengi kuhusiana na maisha ya wokovu, wapo walionisikia na kutendea kazi kile nilichokuwa nimeongea lakini pia wapo wale waliokaidi kwa kuniona mbabaishaji tu.

Kazi kubwa niliyokuwa nimeifanya katika kipindi hicho ilikamilika na hivyo nilitakiwa kuondoka pale shuleni kama walivyoondoka wengine miaka ya nyuma na kuwapisha wengine.
Niliizoea shule na mazingira yake, mbali na hayo, niliwazoea wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wa pale shuleni, kwa hiyo siku ya kuaga, nilijisikia maumivu mno moyoni mwangu.

AZIDISHA UTAKATIFU
Nikarudi nyumbani huku nikisikilizia matokeo ya kidato cha nne. Unajua kwa wanafunzi wengi waliookoka, katika kipindi kama hiki ndicho ambacho utakatifu unaongezeka kwa kuona kwamba endapo ukifanya hivyo basi Mungu ataweza kukuangalia kwa jicho la tatu na wewe upate kitu fulani.

Kwangu, kipindi hicho kilikuwa cha utakatifu sana, nilikuwa muombaji lakini niliongeza zaidi. Kila nilipopiga goti, nilimuomba Mungu kuhusu matokeo yangu, nikawaombea wasahishaji wote, yaani wale wote waliokuwa wakihusika katika harakati zote mpaka matokeo yatoke.

AHOFIA KUFELI
“Nikifeli je?” nilijiuliza huku nikionekana kuwa na hofu.
“Ila ni kawaida tu, kwani nitakuwa wa kwanza kufeli?” Nilijijibu na kujiuliza.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu. Kwa mtu yeyote aliyeokoka ni lazima atakuwa katika vita vikali sana kwa saa ishirini na nne. Ukiona kwamba unaishi maisha yasiyokuwa na vita kutoka kwa shetani basi jua kwamba haujasimama kisawasawa.

APATA VIZINGITI VYA SHETANI
Shetani hataki kabisa kutuona tukimuabudu Mungu, kila siku hutamani kuona akiabudiwa yeye kitu ambacho hujitahidi sana kuanzisha vita na watakatifu ili aweze kuwateka wengi.
Ndivyo ilivyokuwa kwangu, wakati Mungu akinipa moyo wa kuendelea kusonga mbele, naye shetani alikuwa akiniwekea vizingiti vingi.

Niliposema kwamba nitapita hapa kwa msaada wa Mungu, shetani alikuwa akija na kuniambia kwamba kupita lilikuwa jambo gumu sana, hivyo nilitakiwa kurudi nyuma.

AKEMEA SHETANI
Kupambana naye ilihitaji msaada wa Mungu kwani sisi kama sisi hatuwezi kupambana naye. Nilichokifanya ni kuikemea sauti ile ya yule muovu kwani niliamini kwamba maombi ndiyo yalikuwa silaha yangu kuu kumshambulia.

Siku ziliendelea kukatika, presha ya kusubiria matokeo ilikuwa kubwa kuliko kipindi cha nyuma. Hiyo, kwangu ilionekana kuwa nafasi pekee ambayo ingeweza kuwabadilisha wazazi wangu na kuniona kwamba kufeli kwangu darasa la saba hakukumaanisha kwamba sikuwa na akili, hapa, nilikuwa nayo ila ilitokea tu.

WATIANA MOYO
Kwa wanafunzi tuliokuwa tumeokoka, mara kwa mara tulikuwa tukiitana na kuanza kuombeana kwani kila mtu, hasa majirani zetu walitaka kuona kama tungefaulu au la.

“Tutafaulu mitihani yetu na kusonga mbele, mmesikia?” niliwaambia wanafunzi wenzangu ambao tulikuwa tukishirikiana kwenye maombi.“Tumesikia, cha msingi ni kuwa na imani juu ya matokeo hayo kwani Mungu wetu ni muweza wa kila kitu,” alisema Neema.

“Kama kusoma, tumesoma sana, na hata kama kuomba pia tumeomba sana, sasa hivi tusubiri tuone Mungu atafanya nini,” niliwaambia.
“Ila kama ikitokea tumefeli?”

“Hilo si tatizo, yatupasa tukubaliane na kila kitu,” nilisema.
Wanafunzi wengi waliokuwa na uhakika wa kufaulu mitihani yao, na inapotokea wamefeli, huwa hukaa katika hali ya kinyonge na mwisho wa siku kujinyonga. Hatukutaka kitu hicho kitokee katika maisha yetu kwa kuamini kwamba kujiua zilikuwa ni hila za muovu shetani hivyo tulitakiwa kuzishinda.

“Nadhani tunatakiwa kuikemea roho ya mauti,” alishauri Neema na hapo ndipo tulipoamua kuikemea roho hiyo.Maisha yangu yaliendelea kuwa ya kumtegemea Mungu, niliishi kitakatifu huku nikiendelea kwenda kanisani na kumuimbia yeye. Niliyaona mabadiliko makubwa ya kiroho maishani mwangu hali iliyonifanya niendelee kumuabudu kila siku.

Mungu hapendi kuona shetani akiwatesa watu wake kwa magonjwa mbalimbali, Mungu hapendi kuona watumishi wake wakiishi katika maisha ya kimasikini na wakati kwenye Kitabu cha Hagai 2 mstari wa 8 amesema: “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu.”

Ikiwa kama shetani anaweza kuwapa utajiri na kuwalinda watu wake wanaomtumikia, vipi kuhusu Mungu wetu tunayemuabudu? Katika maisha yangu siku zote huwa ninamtumaini Mungu kwa kuwa yeye ni muweza wa yote na mlinzi wa maisha yangu.

MATOKEO YATOKA
Baada ya miezi kukatika, matokeo yakatoka. Kila mtu akawa na presha ya kutaka kujua ni nani kafeli na nani kafaulu. Kwangu, sikuwa na tatizo, matokeo yote ambayo yangekuja kwangu, ningeyachukulia kama yalivyokuwa.

“Nasikia matokeo yametoka,” aliniambia Neema.
“Vipi? Tumefaulu?” Niliuliza huku nikiwa na hamu ya kutaka kufahamu.
“Mmmh! Bado sijajua, subiri,” alisema Neema.
“Wamebandika shuleni?”“Bado. Nafikiri wakiyapata, watabandika,” alisema Neema.

PRESHA YAPANDA
Hapo ndipo ambapo presha yangu ilipoongezeka. Kila nilipokuwa nikikaa, niliyafikiria matokeo hayo kiasi kwamba nikakosa raha kabisa. Baada ya siku chache, matokeo ambayo yalisikika kama tetesitetesi yakabandikwa shuleni, sikuwa nimefanya vizuri jambo lililoninyong’onyeza sana.

Nilirudi nyumbani huku nikiwa kama mtu niliyechanganyikiwa. Siwezi kukuficha, nafikiri hiyo ndiyo ilikuwa siku niliyochanganyikiwa mno, sikuamini kama kumtumikia Mungu kwa miaka yote hakuwa amenifanikisha kufaulu mitihani yangu miwili.

“Mungu, kwa nini hii inatokea kwangu? Kwa nini umeniacha niaibike? Kwa nini umeiacha aibu hii usoni mwangu?” nilimuuliza Mungu. Siku hiyo, nililia mno, sikujua kama katika yote aliyokuwa ameyafanya, yalikuwa ni njia moja ya kuniinua na kuniweka hapa nilipo sasa.
CREDIT:GPL

ITAENDELEA WIKI IJAYO!

No comments: