ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 31, 2014

WENGI TUMEINGIA ‘CHOO CHA KIKE’, TUMEPENDA PASIPO NA PENZI!

Niwiki nyingine tulivu tunakutana tena kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku.Kwa wale wenzangu Waislam naamini watakuwa wameisherehekea Sikukuu ya Idd kwa furaha na amani.
Mpenzi msomaji wangu, wiki iliyopita kama utakuwa na kumbukumbu nzuri niliandika mada iliyokuwa inahusu jinsi unavyoweza kusherehekea sikukuu wakati mpenzi wako akiwa mbali na wewe.

Ni mada iliyowagusa wengi, nashukuru kwamba baadhi tumezungumza kwa simu na wengine tumechati zaidi katika kuwekana sawa pale ambapo mlikuwa hamjaelewa vizuri.

Baada ya kusema hayo, nirudi sasa kwenye mada ya wiki hii. Hivi ulishawahi kukaa chini na kujiuliza kwamba, kama yasingekuwepo mapenzi tungeishi vipi? Kimsingi sipati picha, ni sawa na kujiuliza kama wasingekuwepo wanawake duniani, hali ingekuwaje?
Ninachoona mimi maisha yasingekuwa matamu na huenda ndiyo maana Mungu akatuwekea mapenzi lakini akaona hayawezi kuwepo mapenzi ya jinsi moja ndipo akaumba wanawake na wanaume.

Ninachotaka kukizungumzia leo ni kwamba, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kusema hawatajihusisha nayo na ni bora waishi peke yao.

Wewe msomaji yawezekana ulishawahi kumsikia mtu akisema: “Kwa jinsi yule mwanaume alivyonitenda, sitamani tena kuwa na mpenzi, yaani ni bora niishi peke yangu.”

Mtu anayeweza kutamka maneno hayo ni yule aliyetendwa kwa kiwango cha kupitiliza. Huenda amesalitiwa sana, akavumilia lakini mwisho uzalendo ukamshinda, akamuacha aliyekuwa naye, akampata mwingine.

Huko alikokwenda nako anakutana na mambo mazito zaidi, akasalitiwa, akadharauliwa na kunyanyaswa kiasi cha kutoona faida ya kuwa na mpenzi.

Wengi waliopita kwa wanaume zaidi ya mmoja kisha wakakosa mapenzi waliyotarajia, huishia kukata tamaa ya kuwa na wapenzi na hawa ndiyo wale wanaofikia hatua ya kuapa kwamba hawawezi kupenda tena.

Swali ni je, yupo mtu anayeweza kuishi peke yake bila mpenzi na maisha yake yakawa na furaha? Je, wale walioapia kuwa hawawezi kuingia tena kwenye ulingo wa mapenzi kwa kuwa wametendwa sana, wamefanikiwa kuwa kivyao hadi leo?

Mimi sina uhakika kama yupo ambaye amefanikiwa kuwa singo’ kwa kipindi kirefu cha maisha yake. Wengi ambao nawafahamu waliowahi kutamka maneno hayo leo hii wameolewa na huwezi kuamini wanaishi maisha ya furaha na amani.
Viapo vyao kwamba wasingekuja kupenda tena vimebaki historia. 
Hicho ndicho kilichonisukuma leo kuandika makala haya kwamba, ukiingia kwenye mapenzi, ukaumizwa, huna sababu ya kujiuliza mara mbilimbili cha kufanya, uamuzi sahihi ni kutoka na kuangalia mtu mwingine ambaye atakufanya uyafurahie maisha ya kimapenzi.

Hata kama utaacha au kuachwa zaidi ya mara tatu, usifikie hatua ya kusema hutaki tena kupenda. Kumbuka kupenda kunakuja ‘automatikale’. Leo utamuacha huyu ambaye kakusaliti lakini kesho utakutana na mwingine, atakuvutia na utahisi yeye ni tofauti na yule kumbe ni walewale.

Kikubwa hapa ni kuwa makini na kila unayetokea kumpenda. Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, ni bahati sana kumpenda mtu ambaye naye anakupenda. Wengi wetu tunatokea kuwapenda watu ambao hawatupendi kisha tunawalazimisha watupende kwa gharama yoyote.

Matokeo yake sasa hatudumu. Tunasalitiwa na kuachwa kwa makosa madogo yanayovumilika. Yote hii ni kwa sababu tumeingia ‘choo cha kike’ kwa kupenda pasipo na penzi.

We’ jaribu tu kufuatilia utagundua wengi waliongia kwenye ndoa wapo na watu ambao si sahihi. Na hii ndiyo inasababisha michepuko kuwa mingi, migogoro isiyo na maana na talaka sasa imekuwa ni kitu cha kawaida kabisa.

Kutokana na hilo ndiyo maana leo hii kila anayeanzisha uhusiano na mtu, mguu mmoja nje, mwingine ndani. Anajua wakati wowote kinaweza kunuka na wakaachana na hata akiachwa au akiacha, hataumia sana kwani ni jambo alilotarajia.

Ndiyo maana tunasema mapenzi ya sasa ni sawa na kucheza kamari. Unajua unaweza kula au kuliwa. Na mjanja siku zote akiliwa kwenye kamari mara moja hawezi kuacha kucheza, ataendelea hadi pale atakapokula. Kwenye mapenzi nako hivyohivyo.
Akikuumiza huyo uliyenaye, chukulia ni hali ya kawaida kisha jipange tena kuingia kwenye uhusiano na mtu mwingine hadi pale utakapofanikiwa kumpata yule ambaye ni sahihi kwako.
Credit:GPL

No comments: