ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 29, 2014

Askofu: Chikawe hana ubavu wa kulifunga Kanisa Moravian

Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian nchini, Alinikisa Cheyo. Picha na Maktaba

Mbeya. Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian nchini, Alinikisa Cheyo amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe hana ubavu wa kulifuta kanisa lake.
Cheyo alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Chikawe kutishia kulifuta kanisa hilo na madhehebu mengine yatakayoendekeza migogoro.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye maombezi ya kuliombea Taifa yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam juzi, Chikawe alisema Kanisa la Moravian lina migogoro inayosababisha hata waumini wake wapigane hadharani wakati wa ibada.
“Ninawataka viongozi wa kanisa hili kumaliza tofauti zao kupitia mabaraza yao ya ndani badala ya kufikishana katika vituo vya polisi, vinginevyo nitachukua hatua ya kulifuta kwa kuwa yanahatarisha amani ya nchi,’’ alinukuliwa akisema Chikawe.
Kutokana na kauli hiyo, Askofu Kiongozi huyo alijibu jana akisema: “Waziri hana uwezo wa kufuta kanisa kwani ni la Mungu, lakini migogoro itamalizwa na sisi wenyewe.”
Kwa kipindi kirefu kanisa hilo limekuwa na migogoro maeneo ya Tabata na Mwananyamala, Dar es Salaam na Jimbo la Kusini Mbeya.
Hivi karibuni, wachungaji na waumini wa kanisa hilo katika Jimbo la Mbeya walifunga lango kuu la kuingia makao yake makuu na kusababisha polisi na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigala kuingilia kati.
Kutokana na mgogoro huo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, ilifanya kikao cha dharura na halmashauri ya kanisa hilo na ilidokezwa kwamba walifikia mwafaka mzuri.
Hata hivyo, baada ya siku mbili kanisa hilo liliwasimamisha kazi wachungaji watano ambao nao kupitia kwa wakili walitoa siku saba kwa makamu mwenyekiti aliyeandika barua kuwarudisha kazini haraka.
Hivi karibuni, askofu huyo kiongozi aliliambia gazeti hili kwamba sababu za migogoro ndani ya kanisa lake ni utovu wa nidhamu na watu wachache kutaka madaraka.
Mwananchi

No comments: