Wasema hana ubavu kuingilia katiba yao
Wasisitiza Mbowe, Slaa ruksa kugombea
Wasisitiza Mbowe, Slaa ruksa kugombea
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na Uratibu wa Kanda wa Chadema, Singo Kigaila, alisema msajili wa vyama vya siasa hana mamlaka wala sheria yoyote ya kuwazuia viongozi wanaomaliza muda wao kugombea tena.
Kigaila alisema nafasi zote zipo huru kwa viongozi hao kugombea tena, kwani katiba yao inawaruhusu na kwamba, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa haiwezi kuingilia masuala ya katiba katika chama.
“Hatuna barua ya msajili inayokataza kiongozi kugombea. Ila katiba ya Chadema ndiyo inayoamua. Hivyo, msajili hana mamlaka yoyote ya kusema nani agombee na nani asigombee,” alisema Kigaila.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, hawana sifa za kugombea tena uongozi wa chama hicho kwa kuwa wanabanwa na katiba yao.
Kwa mujibu wa Nyahoza, vyama vyote vinapofanya mikutano huipelekea ofisi hiyo muhtasari, hivyo Chadema nacho kilipeleka kumbukumbu ya mkutano mkuu wa mwaka 2006, lakini hakuna sehemu yoyote iliyoondoa ukomo wa uongozi.
"Hivyo, hawa tayari wana vipindi viwili. Wakichaguliwa katika uchaguzi unaokuja hatutawatambua. Wakitaka, wabadili katiba kwa njia halali, ambayo ni ya mkutano mkuu na si vinginevyo,” alisema.
NIPASHE iliwasiliana na Mbowe kwa njia ya simu kutaka kujua iwapo atatetea nafasi yake katika chama hicho au la, alisema: “Nipe muda nitakuambia.”
Kwa mujibu wa Kigaila, uchaguzi ngazi ya taifa unahusisha mwenyekiti, makamu mwenyekiti upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, ambao wanatarajia kuchaguliwa Septemba 14, mwaka huu.
Alisema uchaguzi huo utafuatia ule wa katibu mkuu na naibu wake siku inayofuata.Viongozi wengine wanaotarajiwa kuchaguliwa ni pamoja na wale wa ngazi za wilaya, majimbo na mkoa kati ya Agosti 15 hadi 30, mwaka huu baada ya kukamilika kwa chaguzi za chama hicho ngazi za kata, vijiji, shehia na nyumba kumi.
Uchaguzi huo pia utahusisha viongozi wa mabaraza ya chama hicho ambayo ni pamoja na Baraza la Vijana (Bavicha), Wazee na Wanawake (Bawacha) ambalo uchaguzi wake utafanyila Septemba 11 mwaka huu.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Naomi Kaihula, aliwataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo ili kujenga uwezo wao na siyo kuonekana kuwasaidia wanaume.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment