Kama ni serikali tatu vigumu kufanyika kama ilivyotarajiwa
Alisema hatma za chaguzi hizo zinategemea matokea ya mchakato wa Katiba ambapo kama yatakuwa serikali tatu itakuwa vigumu kufanyika kama ilivyotarajiwa.
Aliyasema hayo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake katika wilaya za Kilindi, Lushoto, Mkinga na Pangani, mkoani hapa.
"Nilazima hili niliseme kuondoa mkanganyiko, kama itakuwa serikali tatu hakuna uchaguzi,..Uchaguzi wa mwaka huu ni wa serikali mbili kama ilivyo kawaida, zaidi ya hapo itakuwa ngumu kufanya uchaguzi huo," alisema.
Rais Kikwete alisema miongoni mwa mambo yatakayokwamisha uchaguzi mkuu ujayo ni suala la serikali tatu kwani matokeo hayo yatahitaji muda mrefu kufanya maandalizi ya kuruhusu kufanyika kwake.
Alisema kuwa kupita hoja ya serikali tatu ni lazima ufanyike mchakato wa Katiba yake, jambo ambalo alidai kuwa haliwezekani kulingana na muda uliopo kikatiba wa kufanya chaguzi za Serikali za Mitaa, Oktoba mwaka huu na mwakani.
Hata hivyo, aliagiza kufanyika kwa maandalizi kama ilivyokuwa kawaida ya chaguzi zote na kwamba endapo serikali mbili zitakubalika kusiwepo na kikwazo katika kuziendesha chaguzi hizo.
"Pamoja na hayo lakini maandalizi yafanyike kama kawaida kama akiba, kama itapita serikali mbili maandalizi yasiwe kikwazo kwa chaguzi hizo kutofanyika," alisema.
Alisema yeye pia hajui hatma ya chaguzi hizo, lakini aliwasihi Watanzania kuvuta subira kungoja matokeo ya mchakato huo na kusisitiza kuwa hata kama lolote kati ya hayo litatokea ni lazima chaguzi hizo zifanyike hata kama si kwa muda uliyotarajiwa.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kukutana tena Agosti 5, mwaka huu kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Katiba mpya ambapo bunge hilo liliahirishwa kuruhusu Bunge la Bajeti.
Hata hivyo, wakati wa kikao cha Bunge hilo maalumu Katiba, kuliibuka mgawanyiko wakati wa kupitia Sura ya kwanza na sita ya Rasimu hiyo kufuatia kuwepo wa suala la serikali mbili au tatu.
Hatua hiyo ilisababisha kuibuka kwa makundi likiwamo la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambalo linatetea serikali tatu na Tanzania Kwanza, linalotetea serikali mbilli.
Akizungumzia suala la ujenzi wa nyumba za NHC, Rais Kikwete aliagiza kila mkurugenzi kuwa na eneo kwa ajili ya shirika hilo kujenga nyumba vinginevyo watakosa kazi.
Alisema inashangaza ujenzi wa nyumba za NHC kusuasua kutokana na halmashauri kushindwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo.
Alisisitiza kuwa ndani ya wiki mbili anahitaji kupata taarifa ya utekelezwaji wa agizo hilo kabla hajachukua hatua kwa watakaoshindwa kupata maeneo ya ardhi katika halmashauri zao.
"Jamani tuwatumikie watu kama hamuwezi kutenga viwanja kwa ajili ya mradi huo hakuna sababu ya kuwepo kazini....najua hamtaki kutoa maeneo kwa kuwa mkandarasi wa NHC hana pasenti, sasa sitaki kusikia na hili nalisema kwa nchi nzima," alisema.
Aidha, alisisitiza uwajibikaji kwa kila kiongozi katika nafasi yake na kuwataka watoke badala ya kukaa maofisini na kusubiri taarifa ambazo amedai kuwa wakati mwingine hawana muda wa kuzisoma.
Kwa upande wa migogoro ya ardhi, wenyeviti wa serikali za vijiji na watendaji alisema ndio chanzo kwa kuchukua rushwa kutokana na kuendekeza njaa na kuwahifadhi watu kinyemela baada ya kuhongwa mbuzi, kondoo ama pesa.
Kwa upande wa tatizo la soko la mazao ya wakulima aliagiza kituo cha wakala wa taifa wa chakula kununua mazao ya wakulima wa Wilaya ya Kilindi na kwamba suala hilo tayari ameshazungumza na Waziri wa Kilimo.
Aidha, Rais Kikwete alihimiza zao la minazi kustawishwa katika mkoa huo na kuahidi kuwa serikali italeta wataalamu kwa ajili ya kuboresha zao hilo.
Alihimiza pia kilimo cha mboga mboga na matunda na kuutaka mkoa wa Tanga kujiendesha kwa mazao hayo ikiwemo matunda ambayo yanastawi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Alihimiza pia suala la ubunifu na kwamba kila kiongozi lazima awe na lengo kwa ajili ya maendeleo, kusimamia elimu ipasavyo pamoja na kueleza msimamo wa serikali wa kutaka kurejesha uhai wa kiwanda cha chuma ambacho sasa hakifanyikazi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment