ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 19, 2014

KANISA LA TAG LATOA PIKIPIKI KWA WACHUNGAJI MBEYA.

Makamu Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Magnus Mhiche akikata utepe kuzindua pikipiki hizo kwa ajili ya wachungaji
Moja ya wachungaji akipokea funguo za pikipiki hizo kwa niaba ya wenzake toka kwa Makamu askofu
Makamu Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Magnus Mhiche akiongea na wachungaji mara baada ya kuwakabidhi pikipiki
WAANGALIZI wa kanisa la TAG jimbo la kusini magharibi wamekabidhiwa pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi Milion 54 ili kuwawezesha kuwafikia waumini wao kirahisi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 ya mavuno ya kanisa hilo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi pikipiki hizo, Makamu Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Magnus Mhiche, katika hafla iliyofanyika kwenye kanisa la TAG Sokomatola jijini Mbeya, alisema hizo pikipiki ni nyenzo ya kumfanya mchungaji kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Alisema katika maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo kumekuwa na mikakati kadhaa ya kuhakikisha Kanisa linavuna na kuongeza idadi ya waumini katika kuelekea miaka 75 mingine hivyo pikipiki hizo ni moja ya kuhakikisha mpango huo unatekelezeka.

Aidha Makamu Askofu alitoa wito kwa Wachungaji hao waliokabidhiwa pikipiki kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa na sio kuzitumia kibiashara kwa kuwapa madereva wa bodaboda bali watumie katika kazi za kanisa pekee pamoja na utunzaji ili zitumike kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa pikipiki hizo ni mali ya Kanisa ambapo Mchungaji akiacha kazi atalazimika kuikabidhi kwa mrithi wake au kiongozi wa Kanisa na sio kuifungia nyumbani kwake kwa madai ni mali yake kabisa.

Hata hivyo alisema kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa mchungaji mmoja mmoja ni lazima wajifunze kuendesha na kupewa leseni kabla ya kukaguliwa na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani ili wajue sheria zote kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.

Baadhi ya wachungaji waliokabidhiwa pikipiki hizo walitoa shukrani kwa kanisa kwa kutambua ugumu wa kazi waliokuwa wakiupata katika kutembelea makanisa yao kutokana na kuwa mbali na ugumu wa usafiri kwa baadhi ya maeneo.

Mchungaji Moses Kaminyoge Mwangalizi wa Mlowo Wilayani Mbozi alisema pikipiki hiyo itamsadia kuyafikia makanisa yake yote kwa wakati muafaka pamoja na kufuatilia maendeleo ya mavuno ya miaka 10 ya Tanzania kwa Yesu kikamilifu.

Naye Mchungaji Paulo Mfwomi mwangalizi wa Tunduma Wilaya ya Momba alisema pikipiki husaidia maeneo ambayo hayafikiki kwa usafiri wa gari hivyo itarahisisha kufika kila eneo kuwatembelea waumini wake.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments: