Washtakiwa wakisubiri kuingia mahakamani.
Tukio hilo lilitokea saa moja na nusu baada ya washtakiwa hao, Venkat Subbaian (57), Appm Shankar (64), Prabhakar Rao (59) na Dinesh Kumar (27) kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kwey Lusemwa.
Washatkiwan hao walipandishwa kizimbani saa 8:07 mchana na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Magoma Magina.
Magina alidai kuwa Julai 20, mwaka huu washtakiwa wakiwa na nyadhifa tofauti kwa makusudi walishindwa kufukia mifuko 83 iliyokuwa na viungo hivyo kinyume cha sheria ya 128 kifungu cha 8 na cha 9 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Magina alidai kuwa katika shitaka la pili, washtakiwa hao walishindwa kupeleka hati ya kumtaarifu kwamba wamefukia viungo hivyo baada ya kutumika kufundishia kama sheria inavyowataka.
Baada ya Magina kusoma mashtaka hayo, Hakimu Lusemwa alisema washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili raia wa Tanzania kila mmoja.
Kabla mahakama haijasikiliza kipengele cha dhamana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Salum Ahmed aliwasilisha hati hiyo ya Nole kutoka kwa DPP akidai anawaondolea washtakiwa hao mashtaka hayo na kwamba hana nia ya kuendelea kuwashitaki.
Ahmed alifafanua kuwa DPP anawaondolea washtakiwa mashitaka hayo chini ya kifungu cha 91 kidogo cha (1) cha CPA kwa kuwa hana nia ya kuendelea kuwashitaka.
Akizungumza na NIPASHE baada ya kuondolewa mashitaka hayo, Wakili wa utetezi, Gaudiosus Ishengoma alidai kuwa inaonekana kuna mbinu kubwa dhidi ya washtakiwa.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya NIPASHE na Ishengoma:
NIPASHE: Je, unadhani ni kwanini mashitaka haya yameondolewa?
Wakili: Mimi ninavyofahamu kama hati ya mashitaka ingekuwa na kasoro wateja wangu wangepata dhamana na baadaye ingewezekana kubadilishwa.
NIPASHE: Kwa hiyo una mashaka yoyote kuhusu kuondolewa hati hii?
Wakili: Ndiyo, nina mashaka inawezekana DPP ana nia ya kuwafungulia wateja wangu kesi yenye mashitaka yasiyokuwa na dhamana ili wakasote mahabusu.
Wakati washtakiwa hao wakifikishwa mahakamani hapo mapema jana, viunga vya mahakama hiyo vilikuwa tulivu huku wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa IMTU wakiwa wamesimama katika makundi wakijadiliana hatma ya wenzao hao.
Magari mawili ya Jeshi la Polisi, aina ya Rav4 lenye namba za usajili T 366 AVG alipanda mshtakiwa wa tatu kwa madai kuwa ni mgonjwa na wengine waliondoka mahakamani hapo kwa Toyota Land-Cruiser lenye namba za usajili KX06EFYna kurudishwa mahabusu ya jeshi hilo.
MUHIMBILI WANENA
Wakati huohuo; Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea mifuko iliyokuwa na viungo hivyo vilivyotelekezwa Mpiji Majohe.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaisha alisema mifuko hiyo imehifadhi chumba cha kuhifadhia maiti ili visiharibike.
“Viungo hivyo, bado viko chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kwamba MNH haihusiki na utupwaji... inautaratibu maalum wa kuvihifadhi viungo vinavyotokana na wagonjwa ikiwa ni pamoja na kutumia mashine maalumu ya kuviteketeza” alisema Aligaisha.
Hata hivyo, alisema mashine hiyo imeharibika tangu Aprili mwaka huu na bado ipo katika matengenezo kutokana na ununuzi wa vipuri kuchukua muda mrefu kukamilika.
Aligaisha alisema baada ya vipuri hivyo kuwasili, ukarabati ulianza lakini wakati wanaijaribu iliharibika tena na kuamua kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Tafadhali rekebisha sentensi hii iliyoko kwenye kipengele cha kwanza. Haeleweki kabisa "Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kuwapandisha kizimbani kujibu mashtaka ya kushindwa kufukia viungo vya binadamu, kisha kuwasilisha ya kuyaondoa na kupeleka nyingine ya mashtaka ya viungo vilivyotumika kufundishia kwa Kampuni Coroner."
Post a Comment