Advertisements

Tuesday, July 22, 2014

Kuwakamata wanaovaa nguo au kubeba mabegi yenye mabaka mabaka ni uonevu.

Kwenye gazeti la leo imetoka taarifa ya jeshi la wananchi TPDF likikataza na kutishia kuwachukulia hatua kali wale wenye kuvaa na kubeba mabegi zenye rangi za mabaka mabaka ambazo wao wanaona zote mali ya jeshi. Kama mwananchi wa Tanzania naona huo ni uonevu wa raia wasio na hatia kwa sababu zifuatazo;
Mosi, Kuharamisha rangi yoyote yenye mabaka mabaka ni kuwanyang'anya haki na uhuru watanzania, Jeshi halijaeleza kwa nini wananchi waadhibiwe wakati hizo nguo/mabegi siyo ya jeshi letu bali yanafanana tu. Ina maana unaweza ukatuhumiwa mwizi kwa kufanana sura na mwizi?
Pili, Hakuna sheria yoyote katika nchi yetu inayosema kuvaa au kuwa na kitu kinachofanana ni makosa hivyo hilo jeshi linafanya makosa linapoamuru tu kana kwamba kila mtanzania ni mwanajeshi.
Tatu, Kama ni kosa lolote ambalo linahitaji usimamizi (enforcement) linatolewa na polisi kulinganisha na sheria zilizotungwa na bunge. Kwa hiyo jeshi limekurupuka kujifanya wao ndiyo wakamataji (police), waendesha mashtaka (prosecutors) na mahakama kwa upande mwingine. Hivyo hiyo itachangia vipigo kwa raia kama ilivyotokea mara kwa raia na wananchi wengi wamepoteza maisha kutokana na vipigo hivyo, mara nyingi jeshi huwa wanajisahau (hasa majeshi kutoka nchi za africa na asia) kwa vile wanakuwa na silaha basi huwa wanajiona kuwa wapo juu ya sheria.
Hizo ni sababu tatu kati ya nyingi ambazo sikuweza kuandika zote. Watanzania tungependa kuona kuwa jeshi letu linafanya mambo makubwa na wala si kukimbizana na vijana ambao kwa kuvaa nguo au kubeba mabegi yanayofanana na yao wanataka kuwaadhibu, jeshi letu linatakiwa liaminike katika jamii, yanayotokea mitaani na kuwahusisha wanajeshi yanasikitisha na kuhuzunisha hasa kwa jamii yetu inayoamini kuwa jeshi lipo pale kulinda mipaka ya nchi yetu badala yake wao ni vinara wa kufanya fujo kwa kupiga raia wasio na kosa kwenye magomvi yasiyo na maana. Kuna mambo mengi ambayo jeshi letu linaweza kufanya ili liwe bora zaidi katika nyanja zote kuliko kupambana na raia. Katika tamko lililotolewa leo na mkurugenzi wa utawala wa jeshi amesema kuwa kuna watu wanavaa mavazi ya jeshi kama kofia, kombati, boots, na mabegi na wameonekana wakihusika kwenye wizi na unyang'anyi, pia kuna wengine wanamuziki wa kufoka foka wanavaa nguo hizo. Napenda nimweleweshe na baadaye kumuuliza huyo afande kuwa kama watu hao ni asilimia ngapi ya wizi wote unafanywa na hao wavaao boots, kofia, mabegi, mashuka au nguo za jeshi? ni asilimia ngapi kati ya wizi wote unaotokea??? Hata kama kuna wizi tulitegemea lingekuwa ni suala la polisi wala siyo la jeshi kusimamia sheria!! Kama nilivyosema jeshi lina kazi yake na ingekuwa vyema liachane na mambo ya raia, polisi tulionao wanatosha kwa sababu wamefundishwa jinsi ya kushughulika na raia siyo ninyi...kumbukeni operesheni tokomeza mlivyoharibu! Au mnatamani na mnataka kufanya mambo ya Egypt? Wapeni uhuru wenye kupiga muziki wa kufoka foka wavae wanavyotaka ili mradi hawajavaa/hawajaiba mavazi yenu, kwani wana haki kama wafanyavyo watu wengine duniani au mtasema na hao wakimaliza video zao wanaenda kuiba. Ninaandika haya kwa sababu ilishanitokea mwaka 1987 nikiwa mwanafunzi wa high school nikirudi nyumbani baada ya likizo tulikuta wanajeshi wengi wakiranda randa jamhuri street, Dar eS Salaam wakikamata watu hovyo kwa kuwa tu na mabegi yenye mabaka mabaka na langu likiwa na mabaka mabaka ilioandikwa US Army, wale waliokamatwa pamoja na mimi, wazee, watoto, vijana, wanawake etc tuliteswa kwa sababu tulikuwa na mabegi yenye mabaka, hadi leo naamini bado jeshi letu linataka kuendeleza ubabe na uonevu, sasa kwa mtindo huu JE HILO NI JESHI LA WANANCHI? lenye kutesa wananchi wake, lililojipachika jukumu la jeshi la polisi la kukamata wananchi wasio na makosa. Tunatakiwa tulikemee jambo hili ambalo kwa mwananchi wa kawaida tu ataona ni uonevu. Kuna mambo mengi ya maana jeshi letu kufanya siyo hilo la kuonea wananchi wasio na makosa, jeshi halipo juu ya sheria tupinge baadhi ya viongozi wetu wanaoshindwa kuliongoza kwa kuliogopa kama waziri mkuu Pinda.


Mwananchi mtanzania.

2 comments:

Anonymous said...

Hatia mkononi, Hivi niulize kuna sheria yyt inayosema hairuhusiwi kuvaa nguo ya kijeshi TZ, sio ngonjera za Jeshi?

Anonymous said...

Hakuna sheria kama hiyo, pia hakuna sheria ya jeshi kukamata watu hata kama wangekuwa wamevaa nguo zao, hiyo ni kazi ya polisi. Wanajeshi hawana ruhusa ya kukamata raia hata kama wana MP police wa jeshi, wanaruhusiwa kukamata wanajeshi wenzao kambini tu SIYO URAIANI! Nimekuwa jeshini JKT kwa mujibu wa sheria mwaka 1990 na sheria zote za kukamata zinaruhusu kukamata wanajeshi walio kambini tu hata raia haruhusiwi kukamatwa akiwa eneo la jeshi wanatakiwa polisi wa kawaida wataarifiwe, lakini kwa vile makambi mengi yapo maporini wanaweza kukamata lakini wanakabidhi kwa polisi wa kawaida.