ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 27, 2014

KWELI MAXIMO HANA NAFASI KWENYE TIMU YAKE KWA WACHEZAJI OKWI NA KIIZA

Kocha Mkuu wa Yanga Mbrazil, Marcio Maximo

Kocha Mkuu wa Yanga Mbrazil, Marcio Maximo, ameuachia uongozi wa klabu hiyo kufanya maamuzi ya kusitisha mkataba wa mshambuliaji mmoja kati ya Emmanuel Okwi au Hamis Kiiza ili aweze kubakia na nyota watano kama kanuni za ligi zinavyoeleza.

Uamuzi huo wa Maximo unaonyesha nyota hao hawana nafasi katika kikosi chake kwani kama kocha alitakiwa kutoa uamuzi kutokana na mfumo atakaoutumia ni mchezaji gani anayemfaa kati ya hao na kisha kutoa mapendekezo kwa uongozi kumbakisha.

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alipopewa jukumu la kurejea kukinoa kikosi hicho, alitangaza mapema kiungo Juan Mata hana nafasi katika timu hiyo kutokana na mfumo wake, hivyo akamuuza Manchester United, kadhalika kocha mpya wa United, Louis van Gaal mapema alianika wazi Patrice Evra hana nafasi hivyo kuagiza auzwe jambo ambalo uongozi umemuuza Juventus.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Maximo hakutaka kujihusisha kufanya maamuzi ya nani aondolewe kwenye kikosi hicho ili Wabrazil, Andrey Coutinho na Geinlson Santos Santana 'Jaja' waweze kupata nafasi ya kuichezea Yanga katika msimu ujao.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Okwi na Kiiza wamekuwa wakiwaumiza 'kichwa' viongozi wa Yanga kwa sababu kila mmoja amekuwa na mchango kwenye timu lakini pia kwa nyakati tofauti anaonyesha usumbufu.

"Pale timu inapowahitaji mmoja lazima aanze kusumbua, hii hali inatukasirisha sana, kila mchezaji ni muhimu na hakuna aliye juu ya mwenzake," alisema kiongozi huyo.

Wachezaji wengine wa kigeni ambao Yanga ina mkataba nao ni pamoja na kiungo, Haruna Niyonzima 'Fabregas' na beki, Mbuyu Twite, wote kutoka Rwanda.

Hata hivyo, wachezaji hao wa kimataifa wanne wa Yanga hawajakutana na Maximo tangu aanze kuifundisha timu hiyo kutokana na kuwa kwenye timu za taifa zinazokabiliwa na mechi za kusaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi kuwania kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika.

Yanga tayari imeshaanza kujiandaa na msimu ujao wa Ligi ya Bara ambao utaanza Septemba 20, mwaka huu.

Klabu hiyo pia inatarajiwa kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayoanza Agosti 8-24, mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.
CHANZO: NIPASHE

No comments: