Baadhi ya Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini
Yanga inaweza kuwa imeshika nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Bara msimu uliopita na kufanya usajili wa kutisha wa Wabrazili wawili katika kikosi chake cha mwakani, lakini timu hiyo ipo nje ya klabu 400 bora za Afrika kwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya viwango vya ubora wa soka iliyitolewa na mtandao wa footballdatabase.com, ni klabu mbili tu kutoka nchini ambazo zimepenya katika orodha hiyo ya Afrika.
Azam, mabingwa wa Bara na Simba iliyomaliza katika nafasi ya tano msimu uliopita ndizo klabu pekee kutoka nchini zikiwa katika nafasi za 300.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Bara msimu uliopita na ikashika nafasi ya pili nyuma ya Azam Aprili ligi kuu ya Bara ilipomalizika, na kukosekana kwake katika orodha hiyo lakini Simba ikajumuishwa kunaweza kuwa ukweli mchungu kwa timu hiyo.
Mtandao wa footballdatabase.com umesema viwango vya klabu hizo vimezingatia matokeo ya mpaka baada ya mechi za Jumapili iliyopita.
Azam katika orodha hiyo ni ya 313 ikiwa na pointi 1249 huku Simba ikiwa nafasi tano lakini pointi mbili tu nyuma ya wauza vyakula vya nafaka wa Chamazi hao.
Orodha ya klabu bora za Afrika inaongozwa na TP Mazembe ya JK Kongo yenye pointi 1614, alama 365 juu ya Azam, na timu ya mwisho ni Real Tamale ya Ghana (1201).
Vigogo Al-Merreikh ya Sudan, Esperance de Tunis ya Tunisia, Raja Casablanca ya Morocco na Al Hilal Omdurman ya Sudan vimeingia katika orodha ya timu tano bora za mtandao huo Afrika.
Vita Club ya JK Kongo, Cotonsport ya Cameroon, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Sauzi pia zinakamilisha 10 bora ya timu za Afrika, kwa mujibu wa footballdatabase.com.
Yanga ambayo ilicheza Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa kwa matuta na Al Ahly kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu, itawakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika mwakani.
Azam, ambayo ilinusa na kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika mapema mwaka huu, itacheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment