Advertisements

Monday, July 28, 2014

Malecela: Siku 60 hazitoshi kukamilisha Katiba Mpya

Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amesema siku 60 zilizotengwa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kabla ya kupelekwa kwa wananchi hazitoshi kwa kazi hiyo.
Akizungumza na katika mahojiano maalumu mjini Dodoma hivi karibuni, Malecela alisema: “Watahitaji siku zaidi…
Nadhani kosa moja ambalo tumelifanya ni la kujaribu kuweka muda maalumu wa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Hata hivyo, huu muda tuliouweka hatukuuweka kutokana na uzoefu wa ama nchi fulani, maana tuangalie nchi zilizoandika katiba zao, tuseme nchi fulani walichukua miezi fulani kwa hiyo sisi itachukua siku fulani. Hebu angalia, kanuni tu zilichukua siku 40 na katika hizi siku 40 walizungumza sura ya pili na sita tu.”
Bunge Maalumu la Katiba litaanza Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma kwa siku 60 kukamilisha awamu ya pili ya mchakato huo baada ya kumalizika awamu ya kwanza mwanzoni mwa mwaka huu.
Akizungumzia mchakato mzima wa Katiba Mpya Malecela alisema: “Bado ninaamini inawezekana tukapata Katiba Mpya kama tutakwenda na moyo wa kusema nipe nikupe na haya mambo ya watu kutoka kwenye mazungumzo unajua mara nyingine tunaangalia hapa tu.
“Nimekwenda katika sehemu nyingine za dunia. Mfano wa Jamhuri ya Ireland na Serikali ya Waingereza ilichukua miaka mingapi wakae chini? Iliwachukua miaka mingi lakini walikaa chini wakazungumza wakafikia mahali walipo sasa hivi hakuna mgogoro.
“Wewe ulifikiria Marekani katika siku hizi itakuwa na ubalozi Iran? Lakini sasa hivi wanafikiria kufungua ubalozi Iran. Kwa hiyo mimi nasema tufuate mifano ya nchi nyingine, tusikate tamaa haraka.
Kuhusu hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi, kususia vikao vya Bunge hilo alisema: “Hawa wametoka naamini bado watu wanaweza wakazungumza nao na nyie vyombo vya habari mkawasaidia kuwatolea mifano mingi tu duniani na kumekuwa na migogoro mahali pengine. “Chukua mfano wa Sudan Kusini miezi miwili, mitatu iliyopita siyo walikuwa wakipigana, huyu Rais anasema yule ni mhaini na yule akatoa vikwazo, mimi siji lazima hiki na hiki kifanyike lakini sasa hivi wako wapi! Si wako wanazungumza na mimi nadhani wanaelekea kuunda serikali ya maridhiano.
“Kwa hiyo sikati tamaa, bado nina hakika kwamba wenzetu waliotoka bado kuna nafasi ya kuzungumza nao kwa kuwapa maelezo na wao watakuwa na fikra zao.”
Alisema kila upande utatoa maoni yake na kufikia mwafaka na kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana.
Kuhusu Tanzania kama inahitaji Katiba Mpya kwa sasa, Malecela alisema: “Mimi hapo nadhani nitawakera kidogo kwa sababu mawazo yangu yako vingine kabisa.
“Suala la Katiba mimi ambaye nimekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa miaka 15 na mara nyingi Katiba zilizokuja ama zimetokana na Tanu au na CCM. Sasa Serikali ya CCM ilileta mapendekezo ya kutunga Katiba Mpya. Nilionana na Tume na nilikaa nao kwa saa mbili kwa hiyo kama ni mawazo yangu niliyatoa huko yote.
“Nafikiri tujaribu kuwa makini. Mradi tumefika mahali tumekuwa na Bunge la Katiba sasa sisi sote hasa viongozi tuliobaki hebu tuwe kama watu wanaoangalia mpira.  “Unajua mpira unaona mchezaji kachoka lakini unasema kimbiakimbia, kumbe mwezako nguvu zimemwishia.
“Tukianza kusema maneno hapa katikati, mimi nikisema watasema unaona hata Malecela kasema... Tuwaachie wenzetu wa Katiba, hawa wajumbe wa Katiba, wakae wazungumze, tutaelewana tu!”
Aliwapongeza wajumbe wa Bunge la Katiba kwa kuendesha Bunge bila kanuni lakini baadaye wakasimama na kujitengenezea utaratibu wao.
“Mfano mdogo, Yanga na Simba unawafungia katika chumba kimoja halafu unawaambia watengeneze sheria za mpira. Watafika mahali fulani wakimuona mchezaji wa Yanga mrefu sana, Simba watasema kwenye kanuni tuweke wachezaji wasizidi futi fulani. Hata hivyo, walifikia mahali fulani wakakubaliana.
Imeandikwa na Frank Sanga, Habel Chidawali na Sharon Sauwa.wa Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Mheshimiwa John, kama kweli waliopewa jukumu hili wanaitakia Tanzania yetu mema na amani, walishakaa muda mrefu sana na wanakula fedha ya walipa kodi. Kama wasingeliiCHAKACHUA wakakubali kuendelea na yale mapendekezo ya kamati sidhani hata kama ingelichukua siku 30(thelathini) nikiw ana maana ya mwezi mmoja. Tusiendelee kuwabembeleza wamepewa siku 60 hawakuikamilisha ifuntwe hadi tena miaka ya mbele cha moto kipo, Lawama zote kwa uongozi wa CCM unaochakachua muundo mzima!!