Malkia wa Swaziland Mheshimwa Nomsa Matsebula akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Ndugu Nurdin Babu mara baada ya helikopta iliyomchukua kutua kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Nyamisati huko wilayani Rufiji ambako alikwenda kutembelea Shule ya Wamanakayama inayomilikiwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA. Tarehe 2.7.2014. Kulia ni Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete.
Mke wa Mfalme Mswati III wa Swaziland Malkia Nomsa Matsebula akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Wamanakayama Dkt. Ramadhan Dau mara baada ya mgeni huyo kuwasili huko Nyamisati tarehe 2.7.2014.
Malkia wa Swaziland Nomsa Matsebula akiwa amefuatana na mwenyeji wa Mama Salma Kikwete akiwapungia wananchi wa Kijiji cha Nyamisati waliofika kumlaki mara baada ya helikopta iliyomleta kutua kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Nyamisati tarehe 2.7.2014.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete akimshuhudia Malkia wa Swaziland Nomsa Matsebula akiweka saini kwenye kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Shule ya Sekonadri Wamanakayama.Mwanafunzi Assia Idd akimwonyesha Malkia Matsebula kutoka Swaziland namna ya kutumia i-pad kwenye masomo ya sayansi na hesabu wakati Malkia huyo alipotembele Shule ya Sekondari ya Wamanakayama inayomilikiwa na Taasisi ya WAMA inayoongozwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.Malkia wa Swaziland Nomsa Matsebula akipanda mti wa kumbukumbu ya kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Wamanakayama iliyoko katika Kijiji cha Nyamisati
katika wilaya ya Rufiji.
Mke wa Mama Salma Kikwete akimpokea Mgeni wake Malkia wa Swaziland Nomsa Matsebula mbele ya jengo la ofisi ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA.Mama Salma Kikwete akimkabidhi mgeni wake zawadi ya picha.
wanafunzi Elizabeth Kipoto anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya wasichana ya Wamanakayama akiwaonyesha wageni jaribio la kujua kama kuna protini kwenye vyakula katika maabala ya Biologia shuleni hapo. PICHA NA JOHN LUKUWI
Mke wa Mfalme wa Swaziland Malkia Nomsa Matsebula ameipatia shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani zaidi ya shilingi milioni tano ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo katika mahitaji yao ya kila siku.
Malkia Matsebula ambaye ni Mke wa Mfalme Muswati alitoa fedha hizo jana wakati alipoitembelea shule hiyo ambayo ni ya bweni inayopokea Watoto yatima na wanaotoka kwenye familia maskini kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Akiongea na wanafunzi hao Malkia Matsebula aliwataka wanafunzi hao kutumia nafasi hiyo kusoma kwa bidii kwani msichana ni mtu anayeyashika maisha yake ya baadaye katika mikono yake kwa kujenga nyumba ya upendo, kufanya kazi zake vizuri kwa kuona jamii yake inakuwa.
Aliwataka kusoma masomo ya aina mbalimbali ili hapo baadaye waweze kuwa na taaluma mbalimbali zikiwemo za ujenzi, injinia ,sheria, uhasibu kwani elimu haitoki katika mti bali ni mpangilio ambao mwanafunzi anajipangia.
“Kumbukeni kuwa Elimu haipatikani shuleni peke yake bali hata katika jamii inayowazunguka kwani kwenda shule siyo kama umeelimika bali unatakiwa kuvifanyia kazi vile ambavyo umejifunza, wanawake onyesheni elimu yenu kwa vitendo ili jamii inufaike na elimu hiyo.
Wanawake ni watu wanaopenda jamii ingawa wanakutana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, kuacha shule, unyanyasaji wa kijinsia kwani bila ya wao hakuna maendeleo katika nchi , nyinyi tumieni nafasi hii kusoma kwa bidii ili hapo baadaye muweze kuzitatua changamoto hizo”, Malkia Matsebula alisema.
Aliwasihi wanafunzi hao kujenga tabia ya kujiheshimu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuongea na kuvaa mavazi ya heshima na kuheshimu wengine kwani Elimu inakuja kwa kujiheshimu.
Aidha Malkia Matsebula aliwaomba wadau wengine wa maendeleo kumuunga mkono Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu jambo ambalo litasaidia kupatikana kwa viongozi na wanawake wengi wasomi hapo baadaye.
Kwa upande wa walimu aliwataka kuwafundisha wanafunzi hao Historia ya nchi yao na Bara la Afrika kwa ujumla ili wajue ni wapi walikotoa na viongozi wao walikuwa wanafanya mambo gani. Kwa kufanya hivyo wataweza kuilinda na kuitetea nchi na bara lao.
Naye Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alimshukuru Malkia Matsebula kwa kutembelea shule hiyo na kusema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kama mtoto wa kike atapata elimu ya kutosha tatizo la ndoa za utotoni, vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vitapungua.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo inayoendesha shule hiyo; alisema walichagua elimu kwa mtoto wa kike kuwa moja ya kazi zinazofanywa na yake kwa kuamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ambayo mwanamke alikuwa ameikosa kwa muda mrefu.
“Taasisi ya WAMA iliamua kujenga shule hii ili kuweza kutoa elimu kwa watoto wa kike ambayo ni yatima na wanatoka katika mazingira hatarishi kwani watoto hawa walikosa nafasi ya kusoma ukilinganisha na watoto wengine”, alisema Mama Kikwete.
Shule hiyo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 hadi sasa idadi ya wanafunzi imekuwa na kufikia 336 na katikati ya mwezi huu inampango wa kuanzisha kidato cha tano na cha sita.
Licha ya kutembelea shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama Malkia Matsebula aliitembelea Taasisi ya WAMA iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo pia alishiriki chakula cha jioni kilichoandaliwa na mwenyeji wake Mama Salma Kikwete
No comments:
Post a Comment