ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 29, 2014

Maswali mengi kuliko majibu mpaka lini?

Joseph Kapinga

Ikifikia wakati kila uamkapo asubuhi unajikuta na maswali mengi ya kujiuliza kuhusu maisha kuliko majibu, hapana shaka kitakachofuata ni kuchanganyikiwa.
Ndivyo medani yetu ya michezo ilivyo. Kila siku tunaamka na maswali mapya ya kujiuliza kuhusu hatima yetu. Tunalimbikiza maswali yasiyo na majibu. Siyo timu za taifa, klabu wala viongozi. Maswali ni kila siku.
Na ukitaka kujaza maswali kichwani mwako, jaribu kuwauliza viongozi wetu, au kosoa utendaji wao. Utaonekana mbaya, mchokonozi usiyestahili kuvumiliwa katika jamii. Ndiyo maisha ya medani ya michezo nchini.
Viongozi wamejisahau. Hawatimizi wajibu wao na hawataki kuulizwa kuhusu lolote kwenye uongozi wa umma. Wanataka kila kukichwa washuhudie wameandikwa vizuri.
Wanataka hata kwenye ubaya wa utendaji wao, waandikwe vizuri, wapambwe waonekana ndiyo viongozi bora. Sasa kwa hali hii, utakosaje maswali mengi ya kujiuliza kuliko majibu?.
Utamaduni wao mbaya wa kung’ang’ania madaraka na kujenga misingi ya kubebana katika kuongoza taasisi na klabu mbalimbali za michezo ni hatari kwa maendeleo ya ustawi wa michezo nchini.
Leo hii kuna viongozi wameganda kwenye uongozi miaka nenda, rudi. Hakuna walilofanya kuletea mafanikio. Shutuma za uongozi mbaya dhidi yao haziishi kusemwa. Zinasemwa asubuhi, mchana na hata usiku.
Na ukitaka kuchafua hali ya hewa, waambie wajiuzulu kwa vile wameshindwa kusimama kwenye mstari wa dhamira ya mafanikio. Watakuwa wakali na kukuhoji kwa nini unawafuatilia sana. Watakuacha na maswali mengi ya kujiuliza kuliko majibu. Ndipo tulipofika sasa katika medani ya michezo. Inashangaza kuona baadhi ya viongozi wakijisahau, hawakumbuki walikotoka. Wameufanya uongozi wa umma kuwa binafsi. Hawataki kukosolewa, wagumu kukubali makosa. Mpaka lini maswali haya?.
Hata kama inatokea wameboronga katika utendaji wao na kutakiwa kuwajibika, hakuna anayeweza kufaya hivyo. Kwa nini wajiuzulu? Halafu aongoze nani wakati vyeo vimeandikwa majina yao?.
Nikumbushe. Kiongozi bora ni yule anayefuata misingi bora ya uongozi, atakayekuwa na tafsiri sahihi ya uongozi ni dhamana. Atayeiheshimu katiba na kuifanya kuwa kielelezo bora cha uwajibikaji.
Atakayekuwa tayari kuwajibika ashindwapo kutimiza malengo ya uongozi, atakayeongoza kwa tija ya umma na siyo kinyume chake. Angalau haya yakifanyika tunaweza kupunguza wingi wa maswali. Majibu hayatatusumbua. Na hatari ya kuchanganyikiwa tutajitenga nayo.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Tatizo letu ni kuwa hatujui kama hatujui.Unapozungumzia michezo Tanzania, karibu kila mtu anajua. Ni mpaka pale tutapokubali kuwa hatujui ndipo hali inaweza kubadilika kwa kukubali kujuzwa. Tanzania karibu kila mtu anjua, ukumwambia hajui, mnagombana.