ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 5, 2014

Maximo:sikuja Yanga kuifunga Simba

Kocha Maximo wa Yanga

Siku chache tangu kocha mpya wa Yanga, Marcio Maximo, kuanza programu yake ya mazoezi na timu hiyo, amesema haiandai kwa ajili ya kumfunga mtani wa jadi Simba kwa kuwa hayo si mafanikio ambayo timu hiyo inahitaji.

Kocha huyo Mbrazili wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, anayefahamika kwa misimamo mikali, alisema mashabiki na wanachama wa Yanga wanatakiwa kufahamu mafanikio sio kuifunga Simba bali kufanya vizuri kwenye mashindano ya klabu ya Afrika.

Alisema lazima watanzania wawe na wivu wa maendeleo kwenye soka na wasiishie kufurahia timu zao zinapochukua ubingwa wa Bara au kuwafunga wapinzani wao wa jadi.

"Nafahamu upinzani uliopo nchini, hasa wa Simba na Yanga," alisema Maximo aliyeingia mkataba wa miaka miwili na kueleza zaidi, "lakini lazima niseme jambo hili.

"Naandaa timu yangu kwa ajili ya kufanya vizuri ndani na nje ya nchi na hili linawezekana kama mashabiki na wanachama wataungana na mimi."
Alisema Yanga ni timu kubwa na kwa historia yake inapaswa kuwa moja ya timu zenye ushindani mkubwa barani Afrika.
"Sitafanya kazi kwa ajili ya kuifunga Simba.

"Naandaa timu ambayo itakuwa na uwezo wa kushindana na timu yoyote ndani na nje ya Tanzania."

Aidha, alisema tangu kuanza mazoezi amefurahishwa na wachezaji aliowakuta kikosini ambapo alisema wana uwezo wa kufanya kazi atakayowapa.

"Wachezaji wana ari... nimefurahi na jambo hili na hata kwenye mazoezi wanafuata kile ninawaelekeza japo bado hatujakaa pamoja ndiyo kwanza tumeanza mazoezi," alisema zaidi Maximo ambaye hupenda kusisitiza nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.

Maximo alisema baada ya mazoezi ya kuwajengea stamina wachezaji wake, ataanza kutoa mazoezi ya kiufundi zaidi baada ya wiki moja.

Yanga imeanza mazoezi chini ya Maximo pamoja na msaidizi wake Leonardo Neiva kujiandaa na ligi kuu ya Bara itakayoanza mwezi ujao.

Aidha, timu hiyo itacheza Kombe la Kagame la klabu ibngwa ya Afrika Mashariki na Kati nchini Rwanda baadaye mwezi huu na Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika mapema mwakani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: