ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 5, 2014

Sheikh na mgeni wake wajeruhiwa kwa bomu wakila daku


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas

Sheikh alijeruhiwa miguu yake yote na mapajani huku Kifea akipata majeraha makubwa miguuni na kupoteza baadhi ya vidole vya miguu yote.

Bomu la kutupa kwa mkono, limewajeruhi Sheikh Sudi Ally Sudi (37) nyumbani kwake mtaa wa Majengo Chini wakati akipata daku majira ya saa 5 usiku wa kuamkia jana pamoja na rafiki yake Muhaji Hussein Kifea (38), mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam aliyekuwa akitokea Nairobi, Kenya.

Sheikh huyo wa Msikiti wa Qiblatan uliopo eneo la Kilombero jijini hapa na rafiki yake wamejeruhiwa vibaya maeneo ya miguuni na kwa sasa wamelazwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Wakati Sheikh Sudi ambaye pia ni kiongozi wa Answar suna Kanda ya Kaskazini akiwa amejeruhiwa miguu na sehemu za mapajani, Kifea amejeruhiwa miguuni na kupoteza baadhi ya vidole vya miguu yote miwili.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana. Alisema polisi wameanza kupokea taarifa ambazo wanazifanyia kazi ili kuwabaini wahusika.

Alisema watu wasiojulikana wakiwa na bomu la kurusha kwa mkono, walivunja dirisha la nyumba ya Sheikh Sudi na kurusha ndani bomu hilo ambalo liliwajeruhi vibaya.

Akizungumza hospitalini hapo, Sheikh Sudi, alithibitisha kujeruhiwa kwa bomu sebuleni yeye na mgeni wake wakati wakila daku nyumbani kwake majira ya saa 5 usiku.

Alisema kulitokea mlipuko mkubwa wakati bomu hilo liliporushwa sebuleni, huku vipande vya vyuma vikiruka hewani.

Hata hivyo, alidai watu waliofanya hivyo wanafahamika kwa maelezo kwamba siku tatu kabla ya tukio hilo kwani alishawahi kutishiwa kwa njia ya maandishi kuwa atapigwa risasi.

Alisema tukio hilo la kutishiwa maisha aliliripoti kituo kikuu cha polisi cha mkoa, pamoja na kutoa maelezo ya watu wanaowatuhumu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye alifika kumjulia hali hospitalini hapo, kwa mara nyingine alikemea matukio ya ulipuaji mabomu mkoani hapa.

Alisema baadhi ya watuhumiwa wa mabomu hayo wamefikishwa mahakamani na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wengine.

Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema (Chadema), alilitaka jeshi la polisi kurejesha amani jijini hapa kwa kulivalia njuga suala hilo. Alitakaliwahakikishie wananchi kuwa Arusha ni salama kwa kuishi.

Hadi sasa Mkoa wa Arusha umekumbwa na matukio ya kulipuliwa kwa mabomu katika mikusanyiko mbalimbali ya watu.

Mara ya kwanza ilitokea Mei 5, mwaka huu, wakati watu wasiojulikana waliporusha bomu kwenye mkusanyiko wa Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa Parokia ya St Joseph Mfanyakazi Olasiti ambalo liliua waumini watatu wa kanisa hilo na kujeruhi wengine zaidi ya 80 kati yao vibaya.

Katika ibada hiyo Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu, Francis Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu walikuwa miongoni mwa viongozi wa kanisa hilo walionusurika na bomu hilo.

Tukio lingine na mlipuko wa bomu lilitokea Juni 19 mwaka huu, wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata nne za mkoani hapa.

Mlipuko huo ulitokea katika uwanja wa Soweto, ambapo watu watatu walipoteza maisha yao na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa kati yao vibaya.

Hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na matukio hayo. Mlipuko mwingine ulitokea wakati mamia ya wakazi wa hapa wakiangalia matangazo ya mpira yaliyokuwa yakirushwa kwenye runinga katika baa moja ya Arusha Night Park ambapo mtu mmoja alifariki wakati akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Kufuatia tukio hilo watu wanane wamefikishwa mahakamani huku wengine wanane wakishtakiwa kwa tuhuma za kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al shabab.

 

CHANZO: NIPASHE

No comments: