ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 11, 2014

MRC lahusishwa na mashambulizi Lamu

Mashambulizi yalitokea mara ya kwanza katika eneo la Mpeketoni ambapo zaidi ya watu 60 waliuawa
Watu 300 waliokuwa wamejihami wamevamia kijiji cha Pandanguo katika Kaunti ya Lamu Pwani ya Kenya.

Polisi wamehusisha kundi la MRC linalopigania kujitenga kwa jimbo la Pwani na shambulizi hilo na kusema kwamba huenda linapokea ufadhili kutoka kwa makundi ya nje kufanya mashambulizi hayo.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa naibu mkuu wa polisi Samuel Arachi.

Chifu wa eneo hilo Karisa Charo Karisa, anasema kuwa shule na nyumba nne ziliteketezwa katika mashambulizi hayo yaliyofanywa usiku wa kuamkia leo ikiwemo shule moja ya msingi.

Duru zinaarifu kuwa washambuliaji hao walifanya uvamizi saa tatu usiku na kuiba bunduki sita kutoka kwa polisi wa akiba.

Walivamia msikiti ambako polisi hao wa akiba walikuwa wanasali. Mmoja wa polisi hao aliyeponea kifo aliambia BBC kuwa waliambiwa wachague kati ya mauti na bunduki zao.

'Ukatili wa kiwango kibaya'

Hapo ndipo walilazimika kuwapa washambuliaji hao bunduki zao.

Kwa sasa hakuna taarifa zozote kuhusu majeruhi wa mashambulizi hayo.

Inaarifiwa kuwa wanajeshi wamepelekwa katika eneo hilo kudhibiti usalama.

Mnamo mwezi Juni watu watano waliuawa katika eneo hilo la Pandanguo ambalo liko umbali wa kilomita 30 kutoka Mpeketoni ambako mashambulizi mengine yaliwaacha watu zaidi ya sitini wakiwa wameuawa.

Waathiriwa wengi wa mauaji walipatwa wakiwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo na koo zao zikiwa zimekatwa.

Eneo la Lamu ambalo liko Pwani ya Kenya limeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara tangu mwezi Juni huku watu wakiuawa kwa misingi ambayo bado ni tata.

Mashambulizi ya Kwanza yaliyofanyika mjini Mpeketoni, yalisemekana kufanywa na kundi la wanamgambo la Al Shabaab ingawa serikali alilalaumu wanasiasa kuyachochea mashambulizi hayo.

BBC

No comments: