Dar es Salaam. Tanzania imeiomba Serikali ya Uingereza kulirudisha Shirika la Ndege la British Airways (BA) ili lianze tena safari zake hapa nchini kusaidia kukuza biashara na utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa wakati wa mkutano wa pamoja na Waziri wa Masuala ya Afrika wa Uingereza Mark Simmonds, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema tayari wameshawasilisha maombi hayo.
Membe alisema pia waliomba viza ziwe zinatolewa nchini ili ziwarahisishie wasafiri mchakato wa kuandaa safari za kwenda Uingereza.
“Tumewaomba Uingereza warudishe usafiri wa ndege zao nchini ili uwezeshe kuleta watalii wengi na wafanyabiashara,” alisema Membe.
BA liliacha kufanya safari zake za moja kwa moja kati ya Tanzania na Uingereza Machi mwaka jana kwa kile lilichoeleza ni kujiendesha kwa hasara. Kabla ya kusitisha huduma zake, BA ilikuwa likifanya safari zake mara tatu kwa wiki, Dar es Salaam hadi London.
Membe alisema Tanzania imeshajitanua kiuwekezaji na kwamba iwapo shirika hilo litarudisha huduma zake, basi litatanua zaidi uwanja wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Mbali na maombi hayo, Membe alisema tayari kuna mkutano umeandaliwa Novemba mwaka huu utakaoangazia uwekezaji katika sekta ya utalii nchini na kuongeza uhusiano na Uingereza. Kwa upande wake Simmonds alisema wameshafanya makubaliano na Tanzania juu ya mkutano huo na kwamba watahakikisha kuwa kampuni za Uingereza zinashiriki.
Mwananchi
1 comment:
Jamani tuko nyuma kiasi hiki? Kwanini tuombe? Tunaomba serikali ya Uingereza au tuongee na British Airways kuona sababu za wao kusitisha safari hizo? Hii ni biashara sio siasa. Je safari hizo zinalipa? Wataweza competition na KLM, na wengineo? Kuomba tunaweza kuomba sana ila kama shirika liko kwenye hali ngumu ya fedha, linapata hasara, maombi yetu hayatasaidia.
Post a Comment