ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 30, 2014

Mtei: Ugumu wa Nyerere kuiona nchi ilimefilisika uliniondoa BoT

Mzee Edwin Mtei akizungumza na wahariri wa Mwananchi, nyumbani kwake, Tengeru, Arusha.

Hivi karibuni, gazeti hili lilifanya mahojiano maalumu na mwanasiasa mkongwe nchini na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Edwin Mtei nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha. Yafuatayo na mahojiano hayo:
Swali: Wewe ni mmoja wa Watanzania wachache walioaminiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ukapewa wadhifa mkubwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya Tangayika kupata uhuru wake. Ni kitu gani cha kujivunia mbacho ulikiacha Benki Kuu ?
Mtei: Kwa miaka tisa niliyokaa Benki Kuu ya Tanzania nilifanya mambo mengi ikiwamo kufanya mageuzi makubwa ya utumishi. Nilijenga taasisi yenye wafanyakazi ambao wapo huru kujieleza na kwa kuzingatia utalaamu wao.
Nilitafuta vijana wenye uwezo mkubwa na wasomi na kuwaajiri ambao walisaidia sana kuleta mabadiliko makubwa. Mmoja wa vijana hao wakati huo alikuwa ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa na baadaye Jakaya Kikwete,  Daud Ballali na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini na Waziri wa Fedha, Daniel Yona.
Mwaka 1966 nilikwenda Marekani na nikakutana na Ballali ambaye alikuwa bado akisoma Chuo Kikuu (Howard), nilivutiwa na uwezo wake nikashauri asomee masomo  yatakayoendena na uendeshaji wa Benki Kuu ili akimaliza afanye kazi BoT. Kweli baada ya kumaliza masomo yake nilimwajiri Benki Kuu tukafanya naye kazi akiwa mmoja wa vijana wangu hodari sana.
Nakumbuka baadaye Yona aliondoka BoT akapewa kazi nyingine na Mwalimu Nyerere ya kuongoza Benki ya Nyumba (THB) baada ya mimi kumsifia mbele ya Rais Julius Nyerere kwamba ni mchapakazi hodari.
Swali: Ukiwa kijana mdogo wa miaka 32 ulipewa jukumu kubwa la kuwa Gavana wa Benki Kuu, uliwezeje kuepuka vishawishi ya kuingia katika ufisadi kama tunavyoshuhudia leo baadhi ya watumishi wa serikali wanajiingiza katia wizi wa mali za umma?
Mtei: Nilisimamia maadili ya utumishi wa umma, sikuwa na kitu cha kunishawishi kufanya ufisadi. Nilimpenda sana Mwalimu Julius Nyerere ndiyo maana nilifanya kazi kwa nguvu zote kusaidia utawala wake.
 Katika mazingira ya sasa uadilifu umepungua. Hivi sasa viongozi wengi wanashindana kupeleka fedha Uswisi kuficha, badala ya kuwatumikia wananchi.
Viongozi wengi wametanguliza masilahi yao mbele na kujiingiza katika ufisadi na hivyo kushindwa kuwatumikia wananchi. Viongozi lazima waongozwe na uzalendo na kuwahurumia wananchi maskini.
Swali: Unadhani ni nini kifanyike ili maadili ya viongozi yarejee?
 Mtei: Uadilifu ni sehemu ya mahubiri katika dini zote. kiongozi lazima uwe mwadilifu.
Tuliyoyafanya sisi na Nyerere hivi sasa yanaweza kufanyika kama chama kinachojali wananchi kitaingia madarakani ambacho siyo CCM.
Ufisadi utaendelea kama tutaendelea kuwa na serikali ambayo haina dhamira ya dhati ya  kuwapatia wananchi wake maisha bora.
Lazima wananchi wawe wazalendo waipigie kura nyingi Chadema iingie madarakani mwakani ili kumaliza ufisadi nchini.
Kama wananchi wataendelea kupigia CCM kura iendelea kuwapo madarakani kamwe wasitegemee  ufisadi utaisha nchini hii.
Swali: Wakati gani ulikuwa mgumu kwako wakati  ulipokuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ?
Mtei: Wakati mgumu ambao naukumbuka ulikuwa na changamaoto kubwa wakati nikiwa BOT ni baada ya kuisha kwa Vita ya Kagera. Nchi ilingia katika wakati mgumu kiuchumi, hatukuwa na fedha za kutosha kuendesha mambo yetu, fedha nyingi tulitumia kununulia silaha.
Nakumbuka tulikuwa hatuna hata fedha za kununulia shamba lililokuwa likimilikiwa na mwekezaji Kampuni ya Tangayika Planting Company (TPC). Lakini, Mwalimu akinitaka nitafute fedha Hazina za kulinunulia shamba hilo.
Nilitumwa kwenda nje ya nchi kutafuta misaada, wakati huo tulihitaji watu wa kutupatia fedha ili tuweze kuendesha nchi.
Swali: Ni nchi zipi au mashirika yapi ya fedha ambayo ulikwenda kuyaomba misaada hiyo ?
Mtei: Moja ya mashirika ambayo nilikwenda nikazungumza nao ni Shirika la Fedha la Kimataifa  (IMF), ambalo lilishauri kubadilishwe mfumo wetu wa kuendesha mashirika ya umma. Mashirika ambayo yalikuwa yakifanya vibaya kama vile Shirika la National Milling (NMC)  lilitakiwa kubinafsishwa ili lijiendeshe kwa faida.
Pili, walishauri kushusha thamani ya shilingi yetu, ushauri ambao ulikataliwa na Mwalimu Nyerere. Nakumbuka alifanya ziara mkoani Kigoma ndiko alitangaza kuwa hataweza kugeuka kuwa jiwe la chumvi, akimanisha kwamba hatakubaliana na ushauri huo kamwe.
Ingawa baadaye katika utawala wa awamu ya pili ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi mabadiliko yalianza kufanyika.
Swali: Nini kilisababisha wewe kuondoka katika nafasi ya Ugavana ambayo ulidumu nayo kwa miaka tisa?
Mtei: Baada ya kuwaleta maofisa wa IMF pale Ikulu kumshauri Mwalimu namna ya kufufua uchumi, yeye (Mwalimu) hakufurahishwa na ushauri wa kushusha thamani ya shilingi. Alitamka kwamba atashusha thamani ya shilingi labda akiwa tayari amekufa.
Kauli hiyo ilikuwa nzito kwa kiongozi wa nchi ambayo ilinifanya niamue kujiuzulu.  Kauli hiyo ilionyesha wazi kuwa hakuwa akijua kuwa nchi ilikuwa imefilisika. Kwa hiyo katika mazingira hayo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kujiuzulu katika nafasi yangu ya ugavana.
Ilikuwa siku ya mwisho wa wiki niliendesha gari langu mwenyewe kutoka ofisini kwenda nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani akanikaribisha kisha nikamkabidhi barua yangu ya kujiuzulu.
Jioni ya siku hiyo vyombo vya habari wakati huo Radio Tanzania (RTD) na magazeti ya serikali yalitangaza kuwa nimejiuzulu na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Hata hivyo, miezi mitatu baadaye Mwalimu Nyerere aliniteua kuwa mwenyekiti wa Taasisi ya Fedha ya TDFC. Nikiwa katika taasisi hiyo nilifanya ushawishi wingi kwenye taasisi za fedha za nje tukapata misaada mingi.
Baadaye Rais Nyerere aliniteua kwenda makao makuu ya IMF, Wshington  nchini Marekani kufanya kazi nao. Nikiwa huko nitembelea nchi mbalimbali kujifunza masuala ya uchumi.
Swali: Mwaka huu umetimiza miaka 82, ni jambo la kumshukuru Mungu, unatarajia kufanya jambo gani kwa chama chako (Chadema) na kwa Watanzania katika maisha yako yaliyobakia duniani?
Mtei: Nibakie kuwa kisima cha kuchota uzoefu na ushauri mbalimbali kwa Chadema na Watanzania kwa jumla.
Nafurahia maisha ya kustaafu uongozi wa chama , lakini siku zote viongozi yaani katibu mkuu, Dk Wilbrod Slaa  na mwenyekiti, Freeman Mbowe wamekuwa wakiwasiliana na mimi kuomba ushauri mbalimbali.
Ingawa hivi sasa siweze tena kuhudhuria mikutano ya kamati kuu na mingine ambayo mimi ni mjumbe kutokana na hali yangu ya afya,  lakini  huwa wananipa taarifa ya uamuzi uliofikiwa katika  katika vikao hivyo.
Nashukuru kuwa chama chetu bado kipo imara na kitaendelea kuwa imara kuendesha mageuzi makubwa ya kisiasa nchini.
Lakini nashukuru kuwa hivi sasa vijana wengi wamepata mwamko mkubwa wa kisiasa ambao unaonyesha wapinzani kukubalika,  hali ambayo ndiyo njia ya kuingia Ikulu.
Swali: Umefanya kazi na Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu ukiwa katika nafasi ya juu kabisa ya uongozi unamwelezea kiongozi huyo ?
Mtei: Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwadilifu sana , alipenda watu wake. Jambo ambalo nalikumba ni kitendo chake cha mwaka 1968 kuamua kupunguza mshahara wake kwa asilimia 10 ili kupunguza pengo la maskini na wa kipato cha juu.
Kitendo hicho kilinivuta na mimi ambaye nilikuwa napata mshahara wa Sh 5,000 sawa na Mwalimu Nyerere kupunguza kwa asilimia hiyo hiyo.
Nilipunguza mshahara wangu kwa hiari yangu baada ya kuona Mwalimu Nyerere kapunguza wa kwake.
Hata hivyo, watumishi wengine wa ngazi za juu walipunguziwa kwa nguvu na serikali ili kuhakikisha kuwa watu wote hatuna tofuati kubwa mno ya kipato.
Mwalimu alikuwa mtu ambaye akifanya mambo yake kwa ajili ya wananchi wake hakutanguliza mbele masilahi yake kama ilivyo hivi sasa kwa baadhi ya viongozi wa serikali.
Swali: Wewe ni mmoja wa waasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini ukiwa kiongozi wa kwanza wa Chadema. Tangu mwaka 1995 uchaguzi mkuu wa vyama vingi ulipofanyika wapinzani hawajashinda kuingia Ikulu . Unadhani tatizo ni nini ?
Mtei: Wapinzani nchini wanaweza kutwaa dola na kuingia Ikulu mwakani, 2015 bila hata kufanya kwanza mabadiliko kwenye Katiba ya sasa.
Wapo watu wanaojidanganya kuwa katiba ya sasa haiwezi kuwaingiza madarakani wapinzani katika uchaguzi mkuu ujao hao wanapotoka.
Siri pekee ya wapinzani kuingia Ikulu ni kuacha ubinafsi na kuamua kumuunga mkono mgombea mmoja anayekubalika kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kukiangusha chama tawala, CCM.
 Ipo mifano mingi ya ushirikiano wa wapinzani bila kulazimika kuunganisha vyama vyao. Kitu pekee kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni ukomavu wa kisiasa.
Tayari hilo limeanza kule Bungeni ambako tunayo serikali ya kivuli iliyoundwa na vyama vyetu,( Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi) inafanya vizuri na huu ni mfano tosha kwamba kwa umoja wa upinzani tutashinda.
Tumeona jinsi ambavyo waziri kivuli wa fedha, Mbatia (James ) ambaye licha ya kuteuliwa na Rais (Jakaya Kikwete) anaichachafya serikali kwa hoja bungeni.
Lazima tutumie mbinu inayofaa. Hapa ninasema kuna kitu kinaitwa Mtei Technique (mbinu ya Mtei). Hii ni ya kutafuta mtu makini na ambaye anafaa kati yetu, tunamsimamisha kama mgombea wetu, kisha sote tumuunge mkono.
Sisi wapinzani, lazima tukae chini, tukubali kuwa sisi ni wanasiasa wazuri kuliko CCM. Tuwaambie CCM, waache kutupuuza, tuwaonyeshe kuwa tunao uwezo wa kuwaondoa madarakani.
Kwa mfano, nilitumwa kwenda Marekani kumshawishi Dk Kabourou, sisi (Chadema) tukamuunga mkono hata akamshinda Premji (Azim) mgombea wa CCM kule Kigoma.
Swali: Vyama vya upinzani vimekuwa vikikumbwa na migogoro mingi mara kwa mara. Unadhani tatizo ni nini ?
Mtei: Wanasiasa ni binadamu, lazima watofautiane kimawazo na kimtazamo, lakini lazima wavumiliane kwa masilahi na ustawi wa vyama.
 Lakini kamwe wasiruhusu tofauti hizo ziwagawe na kuwasambatisha. Wakumbuke kwamba kila unapotokea mzozo, lazima upo mkono wa mpinzani wako, mkono wa CCM, ndiyo unaovuruga upinzani.
 Wakorofi kamwe hawawezi kuvumiliwa na badala yake watafukuzwa kutoka katika chama.
Swali: Ukawa wamesusia Bunge Maalumu la Katiba nini maoni yako ?
Mtei: Ukawa wanazo hoja za msingi ambazo hazina budi kusikilizwa kwanza.
Wana hoja ambazo ni za wananchi, ni lazima zisikilizwe kwanza na kamwe misimamo mikali haiwezi kusaidia katika kufikia mwafaka wa jambo lolote.
Bunge la Katiba lazima lipate kwanza theluthi mbili ili kufanikisha azma ya kupitisha uamuzi wa kuandika Katiba Mpya na bila Ukawa, idadi hiyo kamwe haitaweza kupatikana na Katiba haitapita.
Mimi siogopi kusema, ninasema tutakwenda kwa wananchi, tuwaeleze kwamba tunataka serikali makini isiyo na doa la rushwa, ufisadi au yenye viongozi walafi na wenye kupenda kutorosha mali, rasilimali kwenda nje ya nchi.
Swali: Hivi karibuni Chadema kimeingia mgogoro na Naibu Katibu Mkuu,  Zitto Kabwe na kumvua nyadhifa zote ndani ya chama. Unazungumziaje mgogoro huo ?
Mtei: Zitto ni kijana mwenye akili nyingi, uwezo mkubwa, ni msomi lakini kasoro yake anasikiliza mambo ya watu wengine. Haya yatamvurugia malengo yake.
MWANANCHI

No comments: