ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 3, 2014

Mwakyembe atema 13 uwanja wa ndege

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akitangaza kuondolewa kwa watumishi 13 katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jana ambao wamebainika kuwasumbua wasafiri kutoka nje ya nchi kwa kuwadai rushwa.Picha na Venance Nestory

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameamuru watumishi 13 kuondolewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuanzia jana saa 6:00 mchana kutokana na tuhuma mbalimbali, hasa za usumbufu wa wasafiri kutoka nje.
“Pamoja na makosa mengine, watumishi hawa wamekuwa wakiwasumbua wageni kwa kuwalenga wasio na kadi za homa ya manjano ambao hutozwa kuanzia Dola 50 za Marekani kisha kupewa kadi hizo bila kupatiwa chanjo,” alisema Dk Mwakyembe katika mkutano na waandishi wa habari aliouitisha ofisini kwake jana kutangaza uamuzi huo.
Dk Mwakyembe alisema watumishi hao kutoka Idara za Kilimo, Afya, Mifugo na Uvuvi wanarudishwa kwenye wizara zao haraka kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni moja ya hatua za kusafisha vitendo viovu kwenye uwanja huo ambao huhusishwa pia na wizi kwenye mizigo ya abiria na njia kuu ya biashara ya dawa za kulevya.
Dk Mwakyembe aliwataja watumishi walioondolewa kutoka Idara ya Kilimo kuwa ni Teddy Mwasenga, Esther Kilonzo, Rehema Mrutu, Mary Kadokayosi, Kisamo Samji na Aneth Kariyanga.
Aliwataja walioondolewa kutoka Idara ya Afya kuwa ni Agnes Shirima, Hamisi Bora, Valeri Chuwa, Elighera Mghase na Remedius Kakulu.
Wengine kutoka Idara ya Mifugo ni Eshi Samsoni Ndosi na Anee Setebe.
“Sihitaji kusikia malalamiko yoyote na iwapo watafanya hivyo nitachukua hatua ya pili ya kuonyesha umma kile kilichobainika kupitia uchunguzi wa kamera za CCTV,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema uchunguzi uliofanywa kwa kutumia kamera za CCTV zilizopo uwanjani hapo umebaini kuwa watumishi hao wamekuwa wakitumia nafasi zao kuwabughudhi wasafiri wanaoingia kutoka Arabuni, India, China na baadhi ya nchi za Asia hivyo kujenga taswira mbovu kwa taifa.
“Wengi wamebainika kukamata bidhaa za kilimo, uvuvi na mifugo na kuzishikilia makusudi, kisha badala ya kufuata utaratibu wa kuzichukua na kuzipeleka kwenye vipimo, wamekuwa wakidai kupewa rushwa ili waziachie, na nyingine wamekuwa wakizichukua na kuzipeleka nyumbani kwao kwa matumizi yao, suala ambalo haliwezi kuvumiliwa,” alisema.
Alionyesha kushangazwa kwake na namna watumishi hao wanavyochukua sheria mkononi na kutaifisha bidhaa za wasafiri kwa manufaa yao binafsi, pamoja na kudai kwamba zinapokamatwa zinakuwa “si bidhaa halali, lakini zinapofika nyumbani kwao huwa halali kwa matumizi yao na familia zao.”
“Kama bidhaa ni mbovu, zinatakiwa kuteketezwa. Sasa hawa wanazishikilia, wanadai wapewe rushwa kisha wanazirejesha kwa wahusika. La sivyo, kama nilivyosema, wanazitaifisha. Hii si sawa na haikubaliki,” alisisitiza.
Dk Mwakyembe alitoa onyo kwa wafanyakazi wengine waliobaki uwanjani hapo, akisisitiza kwamba ameagiza uchunguzi huo kuendelea na hatua kali zaidi zitachukuliwa kwa watumishi watakaobainika kuendelea na vitendo hivyo.
“Nimebaini hawa watumishi wa kilimo, afya, mifugo na uvuvi hawavai sare… lazima wavae sare sasa na kama hawana sare, wavae vizibao vinavyoakisi mwanga. Wasiofanya hivyo watupwe nje ya uwanja na wasiruhusiwe kabisa kuingia,” alisema Dk Mwakyembe.
Aliagiza watumishi waliobaki wanjani hapo kutambua kwamba eneo hilo ni sehemu inayohitaji nidhamu ya hali ya juu na kuwaamuru waache kabisa kuwasumbua wasafiri na kuwadai rushwa, kwa kuwa hatua kali ikiwamo kuwekwa mahabusu kwa uchunguzi zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya hivyo kuanzia sasa.
Kiini cha uchunguzi
Dk Mwakyembe alisema kwamba waliamua kufuatilia nyendo zao baada ya kupata malalamiko kutoka kwa raia wa India, Arabuni, China na nchi nyingine za Asia ambao walilalamikia kutendewa isivyo haki wanapowasili uwanja huo wa JNIA.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Duu.. majina yote ya wachaga..