ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 27, 2014

Mwanafunzi aliyefaulu kidato cha tano `azuiwa` kuendelea na masomo

NA MOSHI LUSONZO
Matukio ya wazazi kuzuia watoto wao wa kike kuendelea na masomo yameendelea kushamiri licha ya serikali kukemea tabia hiyo, ambapo jijini Dar es Salaam mama mmoja anadaiwa kumzuia mtoto wake aliyefaulu kuingia kidato cha tano, kwenda shule.

Mwanafunzi huyo (Jina linahifadhiwa) anayeishi Mbagala Misheni amefaulu kujiunga na Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa ameshindwa kuhudhuria masomo kutokana na kudai kupigwa na mama yake aliyemtaja kwa jina la Yvonne Haule akimzuia kuendelea na masomo.

Akizungumza katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Temeke, alikohifadhiwa msichana huyo, alisema mama yake amekuwa akimnyanyasa tangu wakati anasoma Shule ya Sekondari ya JKT Mgulani.

Alisema alimaliza kidato cha nne mwaka jana na kufaulu kwa alama ya daraja la tatu pointi 26 na kuchaguliwa kwenda kujiunga shule ya Benjamini Mkapa.

"Nilifurahi niliposikia nimefaulu kwenda kidato cha tano, lakini nilipomwambia mama hakuonyesha kufurahi, badala yake alisema hana huwezo wa kunisomesha," alisema binti hiyo.

"Niliwaza sana kwa nini mama ananifanyia mambo hayo ikiwa mimi ni mwanawe, nikijaribu kumuomba ananipiga sana na kunifungia mlango ili nisiingine ndani ya nyumba yake."

Kwa mujibu wa binti huyo, mama yake alimzaa akiwa na umri mdogo na alilelewa na upande wa baba yake nchini Uganda, huko alisomeshwa hadi darasa la saba kabla ya kuhamia Tanzania mwaka 2009 akimfuata mama yake.

AJARIBU KUJIKWAMUA
Alisema katika jitihada ya kutafuta ada ya shule baada ya mama yake kugoma kumlipia, alitafuta kazi katika kampuni moja ya uuzaji wa vifaa vya nyumbani, hata hivyo hakuweza kujinasua baada ya kutolipwa pesa za mshahara.

Alipoona hakuna dalili ya kupata mshahara, aliamua kuondoka na baadhi ya vyombo vya kampuni ili kushinikiza alipwe kitu ambacho kilisababisha akamatwe na kuwekwa rumande kwa siku mbili.

"Nilipotoka rumande nilikwenda kwa mama kumuomba abadilishe mawazo yake, lakini hakuonyesha kunijali alizidi kusema hatatoa pesa zake kwani hata yeye ameishia kidato cha nne na anaendelea kuishi," alisema.

Hata hivyo, katika kutafuta njia ya kuondokana na tatizo hilo, alijaribu kupita katika ofisi mbalimbali za serikali, ambako huko wafanyakazi walimchangia pesa za ada na baadhi ya vifaa vya shule.

UTATA WAIBUKA
Kitendo cha binti huyo kuchangiwa pesa za kulipia ada ya shule, kilionekana kumkera mama yake kiasi ambacho kilimfanya apigwe na kutakiwa amtaje mtu aliyetoa pesa hizo.
Alipoona kipigo kinazidi, alikimbilia Ofisi ya Mtaa wa Bugud, na kufikishwa katika ofisi za Ustawi wa Jamii.

Afisa Mtendaji wa mtaa huo, Ruth Tete, alikiri kupokea malalamiko hayo na kueleza kwamba hata yeye ameshangazwa na hatua aliyochukua mwanamke huyo kumpiga mtoto wake na kumzuia kwenda shule.

"Tulijaribu kuwahoji wote wawili, lakini mama mzazi aling'ang'ania hawezi kumruhusu mwanawe kwenda shule hadi hapo atakapotajiwa mtu aliyetoa pesa za ada," alisema Tete.

MAMA AZUNGUMZA
Akizungumza kwa njia ya simu ya mkononi, Yvonne Haule, alisema kwa masikitiko kwamba mtoto wake ana tabia ya kuzusha maneno na kwamba ana ujeuri iliovuka mipaka kiasi ambacho anadiriki kumpiga pale anapomuonya.

Alisema yeye kama mzazi ana haki ya kumuonya mtoto pale anapoona anakwenda kinyume, lakini kwa binti yake huyo hataki kusikia jambo lolote kutoka kwake.

Alisema amemsomesha binti yake kwa gharama kubwa ambapo alikuwa akilipa ada ya Sh. 700,000 kila mwaka, hivyo anaposikia hataki kulipa ada kwa shule ya serikali anashangaa.

'Mzazi gani anayechukizwa na mtoto wake kufaulu, huo ni uwendawazimu, lakini huyu mtoto wangu anataka watu waamini mimi ni mzazi wa ajabu kabisa, ukweli ninampenda sana mwanangu lakini tabia zake zimekuwa za ajabu siwezi kuzielezea," alisema Yvonne.

Alifafanua kwamba, hata hiyo kazi ya kuuza vyombo alimtafutia wakati anasubiri majibu ili asiingie kwenye makundi mabaya.

Baada ya kupata kazi hiyo, tabia yake ilizidi kubadilika na kuanza kutorudi nyumbani kwao na anapoulizwa anakuwa mkali.

"Kitu cha kusikitisha mwanangu amefikia hatua hadi kutangaza kwamba eti namuonea wivu kwa kuwa amefaulu, inaniuma sana kibaya zaidi sasa hivi akiniona ananisonya na kunitemea mate," alisema kwa sauti ya kilio.

Hata hivyo anasema anamuachia Mungu suala hilo kwani yeye ndiye anafahamu kama anamfanyia vitendo vya unyanyasi mtoto wake.

Kauli ya mama huyo iliungwa mkono na mjumbe wa eneo hilo, Mzee Kabisa, ambaye alisema mara kadhaa alimuita binti huyo kwa ajili ya kumsihi asimdharau mama yake hadi kufikia hatua ya kupigana.

Mjumbe huyo alisema anachofahamu yeye Yvonne, alikuwa akijitahidi kumrekebisha mwanawe, lakini ameshindwa baada ya kila mara kuibuka vurugu.

"Kinachotokea hapa ni ushindani kati ya mtoto na mama yake, huyu binti amekuwa hamuheshimu mama yake na hata kesi zao nilikuwa nazisikiliza mara nyingi kabla ya kuhamia serikali za mita.

SERIKALI YAMSHIKILIA MTOTO
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo, Sultani Mziray, alipozungumza na NIPASHE, alisema wanaendelea kumshikilia mtoto huyo hadi hapo hatua mbalimbali za kuhakikisha anaanza masomo itakapochukuliwa.

Alisema tayari wameshamuhoji mama anayetuhumiwa kufanya vitendo hivyo wakati wanasubiri hatua zingine kuchukuliwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: