Advertisements

Sunday, July 27, 2014

Taharuki ya mabomu yatanda

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange

Ujumbe mfupi wa maneno unaosambazwa kupitia simu za mkononi kuhusu kuwapo kwa mabomu yaliyorushwa kutoka nchi jirani ya Malawi na Rwanda, umezua taharuki.

Kwa mujibu wa ujumbe huo, wananchi wametahadharishwa kuwepo kwa mabomu zaidi ya 30 yaliyorushwa kutoka nchi hizo.

Ujumbe huo unasomeka "Habari zilizotufikia hivi punde. Mtazania yeyote: kaa makini usiokote kitu chochote ambacho una mashaka nacho, kuna bomu zimerushwa toka nchi jirani Malawi/Rwanda zaidi ya 30 zenye uzito usiopungua tani 100 hivyo basi uonapo kitu kipo kama chupa ya chai chenye rangi ya fedha ‘usikiguse ‘piga namba 0756000042.

Ujumbe huo unaendelea kusomeka "SMS hii tuma kwa watu uwezavyo: imetolewa na JWTZ/ LSL5CAMRM: asante. Jambo hili usilichukulie utani.

Baada ya wananchi kadhaa kupiga simu na NIPASHE kuupata ujumbe huo, iliwasiliana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ili kupata ukweli wa ujumbe huo.

Msemaji wa Jeshi hilo, Luteni Kanali Erick Komba, alikanusha uvumi huo na kuwataka wananchi kuondoa hofu ya kuwapo kwa hali hiyo.

Alisema ujumbe huo hauna ukweli wowote na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kupuuza uvumi huo.

“Mwaka jana tulikanusha suala hilo mara tatu na mwaka huu tumefanya hivyo mara mbili lakini bado ujumbe huo unaendelea kusambazwa, kikubwa wananchi waupatapo waupuuze hauna ukweli,” alisema.

Luteni Kanali Komba aliwataka wananchi wanaopata ujumbe huo kuupuza kwa kuufuta badala ya kuwasambazia watu wengine.

Hofu hiyo inatokana na matukio kadhaa ya milipuko ya mabomu visiwani Zanzibar na Arusha.

Wakazi wa miji hiyo ambayo ni ya kitalii ilishuhudia mabomu yakilipuka kwenye ufunguzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu Olasiti mwaka jana, wakati mwezi huu mgahawa wa Vama ulisambaratishwa na watu wanane kujeruhiwa.

Ujumbe huo pia huenda umehusisha mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania, unaoendelea kufukuta.

Kadhalika chochoko za maneno baina ya Rwanda na Tanzania kuhusu waasi wa Intrahamwe wa kundi la FDRL huenda pia ikawa chanzo cha ujumbe huo kuzitaja nchi hizo kurusha mabomu hayo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: