MTOTO Marisela Karoli (14) amewaomba wanaharakati wa masuala ya haki
za watoto kumsaidia ili arudi shuleni badala ya kuolewa kama
anavyolazimishwa na mama yake mzazi, Yohana Binde.
Akizungumza nyumbani kwa
msamaria mwema aliyemhifadhi, mtoto huyo alisema alitoroka kijijini
kwao Idindiri, Tarafa ya Pahi, wilayani Kondoa, Dodoma akikwepa kuolewa.
Mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano katika Shule ya Msingi
Idindiri, alisema mama yake mzazi alipokea mahari ya sh 600,000 kutoka
kwa mwanaume anayetaka kumwoa, aliyemtaja kwa jina la Christian Dodi.
“Mwezi wa tano walikuja nyumbani kuleta barua ya posa, mama
akanilazimisha kuipokea, akasema nikikataa atanipiga. Nikaipokea,
walipoondoka nikampa mama, ndani ya ile bahasha kulikuwa na sh 25,000.
“Mwezi uliopita (Juni) walikuja nyumbani kuleta mahari sh 600,000
mama akapokea,” alisema na kuongeza kuwa Alhamisi ya Juni 12 mama yake
aliwapeleka hospitali ya misheni kupima afya halafu wakaingia parokiani
kuandikisha ndoa, lakini Padri Kalani wa Parokia Katoliki ya Kinyasi,
alikataa kuandikisha ndoa hiyo kwa kuwa yeye (Marisela) ni mdogo.
Kwa mujibu wa Marisela, baada ya mama yake kuona ndoa haitangazwi,
alimtaka aende akaishi na mwanaume huyo hadi atakapokua, ili aolewe.
Alisema Juni 22 wakati wadogo zake wakipata Ekaristi katika parokia
hiyo, alitoroka na kwenda Kijiji cha Keikei anakoishi bibi yake mzaa
mama aitwaye Maria Vicent ambapo alilala na kutoroka alfajiri ya Juni
23.
“Niliamka saa 11 alfajiri nikatoka nje kama nakwenda kujisaidia,
nikakimbilia barabarani, likapita basi la Ibony nikapanda. Sikuwa na
nauli, nikamwambia kondakta anisaidie nauli yangu atapewa na dada yangu
anaishi huku (Dar),” alisema Marisela ambaye ni mtoto wa pili kati ya
sita wa mama yake mzazi.
Alisema baada ya mama yake kugundua ametoroka, alimtuma mtu kumfuata,
jambo alilokataa na kukimbilia mafichoni huku akisisitiza kwamba
anahitaji zaidi kusoma.
Marisela anayeishi mafichoni kwa sasa, alitumia fursa hiyo kuwaomba
wananchi wenye nia ya kumsaidia ili arudi shule wafanye hivyo.
Na Irene Mark
No comments:
Post a Comment