Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma Francis Mtinga amelazimika kuwapa wazee wa kimila kondoo wawili kwa ajili ya tambiko la kuwaondoa nyoka wanaodaiwa kuzuia miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwa simu jana, Mtinga alisema uamuzi wa kuwatoa kondoo hao ulifikiwa baada ya kubaini kuwa makandarasi wanaofanya kazi wilayani humo wamepunguza kasi kutokana na kuhofia nyoka wanaoaminika kuwa wa kishirikina.
Alisema makandarasi wanaochimba mashimo kwa kusimika nguzo za umeme wamekuwa wakikumbana na nyoka, huku wale wanaofukia mabomba ya maji wakijikuta katika wakati mgumu baada ya mabomba hayo kupasuka kila wanapoyafukia ardhini.
Mtinga alibainisha kuwa wazee wanaolalamikiwa kusababisha vioja hivyo wanadai kwamba baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali inapita katika maeneo yao ya kutambikia, hivyo walitoa sharti kuwa ili miradi iendelee lazima wapewe kondoo.
“Wao walikuwa wanataka tuwatambue, nimeongea nao, nimewatambua. Nimewapa kondoo wamechinja tena walikula bila chumvi. Huwezi kupuuza haya mambo, maana vibarua wamegoma kufanya kazi wanaogopa nyoka, sasa kazi inaanza kusuasua,” alisema Mtinga na kuongeza:
“Ni muda mrefu mabomba yalikuwa yanapasuka, watu walikuwa wanalalamika kuwa waliondolewa kupisha ujenzi wa mabomba hayo bila kupewa fidia na wakasema watahakikisha yanaendelea kupasuka. Sasa tumewapa walichokuwa wanataka tuone sayansi yao itaishia wapi.”
Pia alibainisha kuwa ingawa Serikali haiamini katika uchawi, historia inaonyesha kuwa wazee hao waliwahi kukwamisha mambo kadhaa ya kimaendeleo baada ya kukataliwa kupewa kitu walichokuwa wanakitaka na kwamba mpaka sasa mambo hayo hayajapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wao wananchi wanaoishi katika maeneo ambako mradi wa mabomba ya maji umepita, wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa haikuwalipa fidia, hivyo kuahidi kufanya kila njia kukwamisha mradi huo.
Akizungumza wakati wa kutia saini mikataba ya ujenzi wa mifumo wa usambazaji maji katika vijiji vitano vya wilaya hiyo juzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba, Mweshimiwa Rajab alikaririwa na televisheni moja akiwataka makandarasi kwenda haraka kuwaona wazee hao ili kunusuru miradi hiyo isikwamishwe.
Kaimu Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chemba, Robert Mganga akizungumza kupitia televisheni hiyo juzi, alisema imani za kishirikina zinakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo... “Kila wanapochimba shimo badala ya kufukua mchanga wanafukua nyoka,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Dk Lutengano Mwakahesya alisema jana kuwa ofisi yake haiamini katika ushirikina na kwamba mkandarasi yeyote atakayeshindwa kufanya kazi kwa kisingizio cha ushirikina atawajibishwa.
“Sisi tunachojua wakati wa kazi wanaweza kukutana na mwamba au jiwe gumu. Rea hawaamini hizo imani, wananchi wanataka umeme na siyo kitu kingine, kama mhandisi akishindwa kutekeleza mradi tutamtoza faini,” alisema.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment