ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 18, 2014

TAMKO LA KIKUNDI KAZI CHA SERIKALI ZA MITAA CHA POLICY FORUM KUHUSU UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2014

policy forum

Sisi wajumbe wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum, tunaowakilisha zaidi ya Asasi  70 za Kiraia tuliounganisha nguvu zetu  ili kuchangia katika kuifanya michakato ya sera ngazi ya serikali za mitaa kuwa yenye uwazi zaidi, ya kidemokrasia, iliyo shirikishi na yenye uwajibikaji, tunapenda kutoa  mchango wetu katika mchakato huu  muhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2014.  
Tunatambua umuhimu wa serikali za mitaa, ambazo zinalenga kupeleka madaraka kwa jamii au kusogeza madaraka ya kufanya maamuzi kwa wananchi ili kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma kulingana na matakwa ya wananchi.  Tunatambua pia, kwamba mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unategemea mchakato wa katiba mpya ambao umepoteza ratiba yake ya awali ambapo katiba mpya ingezinduliwa tarehe 26 Aprili 2014 na kwa sasa umefika njiapanda na hivyo haijulikani wapi tunaelekea katika uandikaji wa katiba mpya.

Kutokana na ukweli kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa ulitakiwa kufanyika kati ya Septemba na Oktoba 2014 na kutokana na matamko mbalimbali yaliyokwishatolewa na viongozi pamoja na wachambuzi wa masuala ya kisiasa pamoja na wadau mbalimbali na sisi kama wadau katika uongozi wa serikali za mitaa tunajiuliza maswali mengi juu ya hatima ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu.


Tungependa kujua kama wadau wakuu ni lini Uchaguzi wa Serikali za mitaa utafanyika? Kama tunavyofahamu kipindi kama hiki utaratibu umekuwa kwamba kanuni za uchaguzi huwa zinakuwa zimeshaandaliwa na kutolewa ambazo kazi yake kubwa ni kutoa mwongozo na taratibu wa jinsi serikali za mitaa zitakavyoendeshwa hivyo tungependa kujua kama kanuni za uchaguzi zimeshaandaliwa? Na kama zimeshaandaliwa zimeandaliwa na chombo gani? Na ushiriki wa wadau ulikuwaje?
Sisi tunataka kusema kuwa tumeona mkutano wa vyama vya siasa na TAMISEMI uliofanyika Morogoro hivi karibuni ambao tumesoma kupitia vyombo vya habari ulikuwa wa kuandaa kanuni za uchaguzi wa serikali na hapa tunataka kusema kuwa kama wadau toka mashirika yasiyo ya kiserikali hatujashiriki wala kushirikishwa katika mchakato wa kuandaa kanuni.
Sisi kama kikundi kazi cha mtandao ambao unajihusisha na masuala ya serikali za mitaa nchini Tanzania tunaungana na Rais Daktari Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete kuwa Tanzania kama nchi kwa sasa iko kwenye mtikisiko mkubwa kuhusiana na mchakato wa kuandika katiba mpya hivyo haiwezi kuhimili pamoja na mchakato wa katiba na chaguzi mbili kuu, hivyo basi tunapendekeza uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike pamoja na Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015 kama ilivyo kwa Kenya na Zimbabwe.

Kwa  kutambua kuwa TAMISEMI sio chombo mahususi cha kuendesha chaguzi hapa nchini,  pia tunapendekeza uchaguzi wa serikali za mitaa  usimamiwe na kuendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi na kwa sasa tupate nafasi ya kubadilisha sheria za uchaguzi na kufanya maandalizi mengine ili tuwe na chaguzi huru na zenye ufanisi mkubwa.

Taarifa kwa waandishi:
Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana na wafuatao:
·         Mwenyekiti Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa : Hebron Mwakagenda:  theleadership2000@yahoo.com,0713612681

·         Alex Ruchyahinduru   +255 757716333, policy2@policyforum.or.tz

No comments: