Mhe. OMAR Yussuf Mzee, Waziri wa Fedha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiongoea siku ya jumatatu kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa mkutano wa Kilele wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Mawaziri kutoka mataifa mbalimbali wapo hapa Umoja wa Mataifa kuhudhuria mkutano huo ambao unajadili utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millenia ( MDGs), changamoto zake, changamoto zinazoibuka, pamoja na mchakato wa maendeleo endelevu baada ya 2015.
Ujumbe uliofuatana na Mhe. Waziri ukifuatilia hotuba yake, kutoka kulia ni Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, Bi. Amina Shaaban, Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar, Naibu Muwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Mwinyi na Bi. Bihindi Khatibu kutoka Zanzibar
Na Mwandishi Maalum,
New York
Zikiwa zimebakia siku
550 kufikia hitimisho la utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDGs), Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha
kuwa, mafanikio yake katika utekelezaji wa malengo hayo kumetokana na
kujituma kwa serikali ambako
kulivutia washirika wa maendeleo.
Waziri wa Fedha katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Omar Yussuf Mzee ameyasema
hayo siku ya Jumatatu hapa Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika siku ya kwanza ya Mkutano wa
Kilele wa Kisiasa ambao
umeandaliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya
Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC)
Katika Mkutano huu na ambao ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kwa kuzindua
Ripoti Mpya ya mwaka 2014 kuhusu utekelezaji wa MDGs, Mawaziri kutoka
mataifa mbalimbali, wanajadiliana na kubadilishana uzoefu katika Mada Kuu inayohusu changamoto za utekelezaji wa MDGs, namna ya kukabiliana
na changamoto mpya na suala zima la maendeleo endelevu baada ya
2015.
Ni katika kuchangia
majadiliano hayo na akizungumza kwa niaba ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndipo Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee,
alipoeleza uzoefu wa Tanzania katika
kuvutia washirika wa maendeleo baada ya kuwa imeonyesha njia.
“ Kujitoa na kujituma kwa serikali
yetu na viongozi wake kumeifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipige
hatua kubwa katika utekelezaji wa baadhi ya MDGs. Ukweli ni kuwa juhudi zetu
wenyewe zilipata uungwaji mkubwa kutoka kwa washirika wetu wa maendeleo, na wadau mbalimbali yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali, ya
kiraia na sekta binfasi”. akasema Waziri Mzee
Ameyataja baadhi ya
malengo ambayo yamepafa
mafanikio makubwa kutokana na
ushirikiano huo kuwa ni lengo namba moja linalohusu elimu ya msingi
kwa wote, lengo namba tatu kuhusu usawa
wa kijinsia, malengo yanayohusu afya na
mazingira. Ingawa pia alisema kama ilivyo kwa nchi nyingine bado kuna changamoto za
hapa na pale.
Akizungumzia kuhusu
hifadhi ya mazingira kama eneo moja la
utekelezaji wa MDGs, Waziri Omar Yussuf
Mzee, amesema, Tanzania inatambua na kuheshimu hifadhi ya
mazingira kama kiungo muhimu kwa maendeleo endelevu.
Akaongeza kwamba ni kwa
kulitambua hilo, ndiyo maana Viongozi wa Afrika walimkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete dhamana ya
kuongoza Kamati ya Viongozi wa Kuu wa Nchi na Serikali kuhusu mabadiliko
ya Tabia Nchi ( CAHOSCC).
Aidha katika eneo hilo
na hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya
tabia nchi, Waziri ameitaka Jumuiya ya
Kimataifa kujituma katika kulishughulikia eneo hilo na hususani athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa nchi Ndogo za Visiwa
ikiwamo Zanzibar.
Akasisitiza kuwa katika
eneo hilo la mabadiliko ya Tabia Nchi, Tanzania ingependa kuona
panakuwepo na ajenda ambayo itakuwa jumuishi na ya jumla lakini ikiwa na utofauti
katika majukumu.
Kuhusu eneo la
maendeleo endelevu, Waziri amesema, Tanzania inaamini kuwa upunguzaji wa umaskini bado ni
muhimili mkuu wa maendeleo
endelevu baada ya 2015. Akisisitiza kuwa ajenda hiyo lazima sasa ifanyiwe kazi kwa ari na kasi mpya licha ya kwamba bado
zipo ajenda nyingine ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu kama
ilivyoainishwa katika MDGs.
Aidha akasema katika utekelezaji wa malengo mapya ya maendeleo ni vema pia kuhakikisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa ikiwamo misaada ya biashara na ufadhili wa kifedha katika
kusaidia juhudi za kitaifa inaendelea kuwapo
Katika eneo hilo la maendeleo endelevu baada ya 2015 Waziri wa Fedha ameongeza kuwa uaandaji wa ajenda mpya na malengo yake kusiwe kana kwamba zinaelekezwa kwa upande mmoja tu
yaani mataifa yanayoendelea, na kutilia mkazo ukusanyaji wa mapato ya ndani. Kwa kile alichosema, ushirikiano wa kweli wa kimataifa unataka juhudi
za pamoja katika kuumaliza umaskini na njaa kwa wote.
Aidha Tanzania kupitia
kwa Waziri wa Fedha imesisitiza kuwa katika utekelezaji wa tamko la Rio+20 kuhusu “Dunia tuitakayo” ipo haja na umuhimu wa kupunguza pengo kati ya walionacho na wasio nacho, urejeshwaji wa misaada ya maendeleo uliokwama baada ya
mdororo wa uchumi, ubadilishanaji wa teknolojia za kisasa ujuzi na utaalam mbalimbali na
kudumisha ushirikiano na uhusiano wa kimataifa.
No comments:
Post a Comment