ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 6, 2014

Uondoshaji makontena kinyemela...TRA yaumbua kile ilichoficha TPA

Wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ikificha sakata la udanganyifu wa kuondoa makontena bandarini jijini Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato (TRA) imeiumbua na kuthibitisha kuwapo na udanganyifu katika kadhia hiyo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, NIPASHE iliibua sakata la makontena yanayodaiwa kuondolewa bandarini hapo kwa vibali feki kwa kutumia kampuni isiyosajiliwa.

Kampuni hiyo ya Green Trading ilitumika kuondoa mizigo bandarini (release order) baada ya TPA kupokea nyaraka zake na kuzitumia kuondoa kontena hilo.

Akizungumzia sakata hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema makontena hayo yalinaswa baada ya kuonyesha kuna udanganifu kuwa yalikuwa yanapelekwa nchi jirani.

Maelezo ya Kayombo yanafuatia taarifa za gazeti hili zilizokanushwa na TPA kwamba haukuwepo udanganyifu wa kuyaondoa makontena hayo.

Licha ya kanusho hilo, ufafanuzi uliotolewa na TPA ulikiri kuwapo kwa kontena linalodaiwa kukamatwa Chang’ombe.

Taarifa ya TPA ilieleza kuwa kulikuwa na jaribio la kutumia nyaraka za kughushi kuondoa kontena namba PCIU 298647-4 lililokuwa limepakiwa katika gari aina ya Scan namba T 425AAY/T318BXS kwa kutumia nyaraka za kughushi lililofanyika Juni 1, mwaka huu majira ya saa 9 usiku kwa kupitia mlango namba tatu lakini lilizuiliwa na askari wa kikosi cha ulinzi cha bandari.

“Hivi sasa watuhumiwa wote wamekamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi wanamaji na kufunguliwa jalada MUD/RB/208/2004,” taarifa hiyo ilieleza.
Wakati TPA walipohojiwa awali walikanusha kuwapo na sakata hilo.

Kayombo katika maelezo yake alipingana na taarifa hizo za mamlaka ya bandari na kueleza kuwa TRA ilifuatilia na kukamata kontena moja Chang’ombe likiwa linapakua vitenge vya wax ambavyo vilitolewa kwa vibali vya kuelekea nje ya nchi.

“Lakini kontena hilo lilipitishwa likidaiwa linakwenda nje ya nchi na ndipo tulipofuatilia tukabaini udanganyifu huo,” alisema.

Alisema wakati maafisa wa TRA wakilikamata kontena hilo, walipewa taarifa kuwa mteja huyo ana kontena lingine lililokuwa linatolewa bandarini hapo.

“Maaofisa walizidi kufuatilia na kulinasa kontena lingine likitaka kutoka getini na kulizuia kwa ajili ya uchunguzi,“ alisema Kayombo.

Aliongeza kuwa kontena hilo lipo chini ya uangalizi wa forodha na kwamba makontena hayo yaliyokamatwa ni ya mteja ambaye jina lake linahifadhiwa kuruhusu uchunguzi.

NIPASHE Jumapili ilimuhoji Kayombo kuhusiana taarifa kuwa mteja huyo anadaiwa kujaribu kutoa kontena kadhaa kwa njia ya udanganyifu kwa lengo la kukwepa kodi, alijibu;

“Suala hilo bado wanaendelea na uchunguzi kubaini kama kuna kontena nyingine zilizokuwa zikitaka kuondolewa kwa njia ya udanganyifu.”

Kuhusu hatua gani zitachukuliwa baada ya kubainika alikuwa anakwepa kulipa kodi, Kayombo alisema watataifisha makontena yake, kulipishwa kodi iliyokuwa inakwepwa pamoja na adhabu.

Hata hivyo, alisema kiasi cha kodi anachodaiwa kujaribu kukwepa hakijafahamika.

GREEN TRADING KUISHITAKI TPA
Gazeti hili lilizungumza na Meneja wa Green Trading, Frank Mushi, ambaye alieleza kuwa ataichukulia hatua bandari kwa kitendo cha kuitumia kampuni yake katika kufanya udanganyifu huo.

Alisema TPA imemfedhehesha kwa kitendo hicho pamoja na kumuweka mahabusu wakati hana hatia na mchezo huo waliufahamu.

Mushi alisema nyaraka zilizotumika ikiwamo kitambulisho pamoja na nembo ya kampuni yake vimeghushiwa katika kutoa kontena.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa bado kampuni yake haina leseni ya kutoa mzigo bandarini, hivyo sheria haimruhusu kutoa mzigo.

“Lakini wajanja wachache wametumia kampuni yangu kutengeneza nyaraka wakati sina leseni na ni kwanini waghushi nyaraka zinazoonesha wao ni wafanyakazi wa Green Trading wakati wahusika hao wana kampuni yao inayotoa mzigo,” alihoji
Habari za ndani kutoka bandarini hapo ziliieleza kuwa Kampuni ambayo inatuhumiwa kughushi nyaraka na kuondoa makontena hayo imedaiwa kuendelea na kazi bila hatua kuchukuliwa.

Awali ilidaiwa kuwa Kontena hizo ambazo zilikuwa zikitokea China zikiwa zimebeba mzigo wa vitenge inadaiwa wafanyabiashara hao walicheza mchezo mchafu katika kufanya udanganyifu kwa lengo la kukwepa kodi.

Ilielezwa kuwa kontena hizo ambazo ni za wafanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, wanadaiwa kuahidi kiasi cha Sh milioni 100 kwa ajili ya kufanikisha kontena hizo kutoka kwa njia za udanganyifu.

Hata hivyo, kontena hizo ziliandikiwa nyaraka kuwa zinaelekea nchini Kongo na hatimaye mchezo huo kugundulika.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

No comments: