ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 4, 2014

Waliotemwa JNIA mikononi mwa Takukuru

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza kuwahoji na kuwachunguza wafanyakazi 13 wa wizara tatu waliotimuliwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Uwanja wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kuwadai rushwa kutoka kwa raia wanaotoka nje ya nchi.

Aidha, Taasisi hiyo imesema watuhumiwa hao wakishahojiwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine wakithibitika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, (pichani) alipokuwa akizungumza na NIPASHE.


“Suala hilo tumeshaanza kulifanyia kazi ikiwa ni kuwahoji na kuwachunguza watuhumiwa hao na ikithibitika kujihusisha na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na ushahidi watachukuliwa hatua za kisheria,”alisema Dk. Hoseah.

Wafanyakazi hao wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo.

Mwakyembe aliwataja wafanyakazi hao kuwa ni Teddy Mwasenga, Ester Kilonzo, Rehema Mrutu, Mary Kadokayosi, Kisamo Samji, Anneth Kiliyanga ambao wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Wafanyakazi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni Agness Shirima, Hamis Bora, Valeri Chuwa, Elingera Mghase na Remedius Kakulu na watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni Eshi Samson Ndosi na Anne Setebe.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Acheni kuonea walala hoi hawa. Wala rushwa wakubwa wa Nchi wanapeta