
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuzindua Barabara ya Dumila-Rudewa mkoani Morogoro, yenye urefu wa Kilomita 45 iliyojengwa kwa kiwango cha lami. Kutoka kushoto ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli. Picha na Esther Kibakaya
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kufuta ada katika shule zake za sekondari.
Akizungumza na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro na wakazi wa vijiji vya jirani akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Morogoro, Rais Kikwete alisema mpango huo utawezesha wanafunzi kuanza darasa la kwanza hadi kidato cha nne bila malipo.
“Tunaangalia jinsi gani ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali kama namna ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anayeanza darasa la kwanza anakuwa na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunaangalia kuondoa ada hii ambako wazazi wanalipa Sh20,000 kwa shule za kutwa na Sh70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila ya wasiwasi wa kukwamishwa na ada.”
Ujenzi wa Sekondari za kata
Rais Kikwete alieleza kukerwa kwake na kejeli zinazoelekezwa katika shule za sekondari za kata, mpango ulioibuliwa na Serikali yake kwa ajili ya kuongeza wigo wa wanafunzi wanaomaliza shule za msingi kuendelea na elimu ya sekondari.
Alisema pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule hizo kiasi cha kuitwa ‘Yeboyebo’ katika miaka ya mwanzoni, zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio ya jumla ya sekta ya elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.
“Serikali yake iliibua mpango wa ujenzi wa sekondari za kata kwa sababu nafasi za wanafunzi kuingia sekondari zilikuwa finyu. Ni asilimia kati ya sita na 10 ya watoto wote waliokuwa wanamaliza shule za msingi mwaka 2005 walikuwa wanaingia sekondari,” alisema.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alitumia muda mrefu kuelezea historia ya maendeleo ya elimu nchini, mabadiliko ya mwelekeo wa elimu na sera ambazo zimeongoza mageuzi makubwa katika elimu chini ya uongozi wake.
“Kwa miaka mingi, tulikuwa hatukujenga shule mpya za sekondari na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndiyo kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na sera ya shule za kata.”
Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2005 kulikuwa na jumla ya shule za sekondari 1,745; zikiwamo 1,202 za Serikali na sasa ziko jumla ya shule za sekondari 4,576 zikiwamo shule 3,528 za Serikali.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment