Advertisements

Wednesday, August 20, 2014

Kiongozi wa Uamsho kortini kesi ya ugaidi

Dar es Salaam. Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Mselem Ali Mselem na mwenzake Abdallah Said Ali wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwamo la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi.
Pia, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kuwasaidia watu hao ili waweze kufanya vitendo hivyo.
Mawakili wa Serikali, Peter Njike na George Barasa walidai jana kuwa washtakiwa hao walijihusisha na makosa hayo kinyume na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Njike alidai mahakamani hapo kuwa Sheikh Mselem aliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary ili kutenda makosa ya ugaidi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa sababu mahakama ya hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo hadi Mahakama Kuu.
Hakimu Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo, aliamuru washtakiwa hao kupelekwa rumande hadi Agosti 21, kesi itakapokuja kutajwa tena. Mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.
Awali Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) ambaye pia ni kiongozi wa jumuiya hizo na mwenzake Jamal Nooridin Swalehe (38) walifikishwa mahakamani hapo kusomewa mashtaka manne yanayofanana na hayo ya Sheikh Mselem.
Sheikh Ahmed anadaiwa kwa makusudi alitoa msaada kwa Absaloum na Omary ili watende vitendo vya kigaidi. Mwananchi

No comments: