Advertisements

Wednesday, August 20, 2014

Mbita atimiza siku 47 katika uangalizi maalumu Muhimbili

Brigedia Jenerali mstaafu, Hashimu Mbita.PICHA|MAKTABA

Dar es Salaam. Brigedia Jenerali mstaafu, Hashimu Mbita ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN), ametimiza siku 47 akiwa katika chumba cha uangalizi maalumu huku wataalamu wakisema hali yake si mbaya wala si ya kuridhisha.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Hospitali ya Muhimbli (MNH), Aminiel Aligaeshi alisema jana kwamba pamoja na mazingira hayo, Brigedia Mbita ambaye amelazwa katika kitengo cha magonjwa ya moyo bado anaweza kuzungumza.
“Hali yake kwa sasa ni ya kawaida tofauti na ilivyokuwa hapo awali, madaktari wanasema anaendelea vizuri na matibabu na wamekuwa wakiendelea na juhudi za kuhakikisha anarejea katika afya yake,” alisema.
Tuzo ya Mwanamutapa
Wakati akiendelea na matibabu, Serikali ya Zimbabwe imemtunuku Mbita tuzo ya juu nchini humo, iitwayo Mwanamutapa ikiwa ni kutambua mchango wake alipokuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi wa Afrika.
Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari jana zilieleza kuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ndiye aliyetoa tuzo hiyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wa Mbita wa kupigania uhuru wa nchi hiyo.
Tuzo ya Mbita ilipokelewa na mtoto wake, Sheila Mbita katika mkutano wa 34 wa mwaka kwa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika, Zimbabwe mwishoni mwa wiki.
Mwananchi

No comments: