Zingatia pia kuwa lazima kila mmoja ajitume kuufanya uhusiano udumu. Muhimu zaidi ni kwamba mapenzi hayatoshelezi kwa uwajibikaji wa nusu nusu. Yanahitaji nidhamu na utekelezaji wa moja kwa moja kutoka moyoni. Yanayomhusu mwenzi wako ni vema uyabebe kama yako, hivyo ndivyo uhusiano unavyotaka.
Mapenzi yanahitaji akili, utashi na fikra zako bila kusahau nguvu zote katika kuzalisha matunda ya kila siku kwenye uhusiano ulionao. Utata unaoonekana ni ule unaotokana na wenzi kutotimiza matarajio ya kila mmoja.
Kuna msemo kuwa mapenzi hayashindwi ila watu ndiyo hushindwa na mapenzi. Tunarukia kwenye uhusiano bila kuwa na uhakika ni kiasi gani tunawapenda wenzetu na ni kwa kiwango kipi tumejiandaa kubeba majukumu.
Mwisho wa siku tunafeli. Tatizo ni kwamba tunaanzisha uhusiano mpya bila kutatua kasoro zilizosababisha tukashindwa kwenye uhusiano na mtu wa kwanza. Hapo nadhani unaweza kuona kwamba wakati mwingine mapenzi siyo tata ila wenyewe tunayafanya kuwa magumu.
Tuna mambo mengi, ya kifamilia, kikazi, imani, dini, kabila, tofauti za kimtazamo na matarajio ya kila mmoja. Hatuko sawa. Tunapoingia kwenye uhusiano, fikra zetu zinakuwa zimejaa lakini ajabu ni kwamba tunapoingia kwenye uhusiano hatuyapi kipaumbele katika kuyajadili na kukubaliana. Hisia za juu hutupeleka kama vipofu.
Uhusiano wa kimapenzi wa watu wengi huanza pale ambapo mtu anajihisi yupo mpweke na anahitaji kampani. Wakati mwingine inatokea kwa sababu mtu anakuwa anakabiliwa na ‘presha’ ya kuwa na mwenzake kwa kigezo kwamba umri umekwenda. Si kwamba amemuona mtu mwenye sifa anazohitaji.
Umri ni kigezo kimoja lakini inawezekana ikawa mtu anataka kuwa na mwenzake kwa sababu ya msukumo wa nafasi yake kwenye jamii au kimila. Pengine ni dada sasa wadogo zake wameolewa yeye bado yupo tu. Au ni kaka, kwa hiyo kama kiongozi wa familia anaona bora aoe mapema kabla ya wadogo zake.
Kama umeingia kwenye uhusiano kwa sababu ya presha ya aina hiyo, utawezaje kuwa na matunda sahihi? Kichecheo cha uhusiano wa kimapenzi kinapaswa kuwa mapenzi. Mnapendana, kwa hiyo nyoyo zenu zinavutana kuingia kwenye sayari spesho.
Usiwe na papara, angalia mahitaji ya moyo wako, weka mbele matarajio yako. Fikra zako uziweke wazi. Unapotafuta mwenzi hakikisha husumbuliwi na presha yoyote. Jambo ambalo unapaswa kuamini ni kwamba aliye ndani ya mawazo yako utampata kama ukijipa nafasi.
SOMO LETU WIKI IJAYO
Itakuwa ni fursa nzuri kwa mada inayohusu yale mambo ambayo unapaswa kuyafanyia usaili ndani ya kichwa chako kabla hujasaliti. Dunia ya sasa, uchepukaji umekuwa mkubwa sana, tamaa imekuwa sababu ya watu kuamua kuwa na uhusiano pembeni ambao unakuwa siyo rasmi.
Wapo ambao huanza pembeni kama utani lakini hunogewa mpaka kusahau uhusiano wao wa awali. Muktadha wa kuchepuka una mambo mengi, hapo ulipo utakuwa umeshashuhudia mtu aliyenogewa alipochepukia mwisho ndoa ikafuata.
Kuna nyumba nyingi zipo juu ya mawe kwa sababu ya matokeo ya kuchepuka. Baba kuanzisha uhusiano pembeni, akanogewa na kusahau nyumba yake. Mama akabaki na familia, watoto wanahangaika, hawaoni mapenzi ya baba yao, kipato pia ni shida, maisha magumu.
GPL
No comments:
Post a Comment