ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 29, 2014

Machifu sasa waomba utawala wao urejeshwe

Makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samia Hassan Suluhu (kulia) akimsikiliza mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu John Mgemela wa Magu (katikati) na Chifu Ndutu Ndaturu wa Bariadi waliotembelea ofisini kwake bungeni Dodoma juzi kutaka mapendekezo yao umoja huo yaingizwe kwenye Katiba mpya. Picha na Emmanuel Hermany.

Dodoma. Umoja wa machifu nchini juzi uliwasilisha mapendekezo yao katika Bunge la Katiba ukitaka yaingizwe kwenye Katiba inayotungwa.
Machifu hao wamependekeza kurudishwa kwa utawala wa Kichifu na Kitemi ili kutoa nafasi ya kurekebishwa kwa jamii ambayo kwa maoni yao imeanza kupoteza mwelekeo.
Mapendekezo ya viongozi hao wa jadi, yalipokelewa na makamu mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaahidi kuyafanyia kazi.
Wakizungumza mbele ya vyombo vya habari jana, Chifu John Mgemela wa Magu na Agnes Ntuzu wa Bariadi, walisema maoni hayo yalitokana na mapitio ya Rasimu ya Katiba inayoendelea kuboreshwa na Bunge hilo.
“Tunataka Katiba ieleze wazi kuwa sera na sheria zitakazotungwa zihakikishe kunakuwa na tume ya taifa ya utamaduni itakayoanzishwa kisheria kusimamia masuala ya utamaduni,”a lisema Chifu Mgemela.
Alisema ni vyema Katiba ijayo ikatoa fursa kwa machifu na watemi kutambulika katika mfumo rasmi wa uongozi wa jamii, ili wasaidie kudhibiti mwenendo wa jamii ambao kwa sasa umepoteza mwelekeo kimaadili.
Akipokea mapendekezo hayo, Suluhu alisema ingawa Bunge hilo halifanyi kazi ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya kukusanya maoni, hawawezi kukataa kuwapokea wananchi wanaopeleka mapendekezo yao.
Alisema muda mfupi baada ya kukutana na machifu hao, ratiba ilikuwa inaelekeza kuwa kamati ndogo ya uongozi wa Bunge hilo ikutane na miongoni mwa kazi ambazo zingefanywa ni kujadili mapendekezo yaliyopokelewa.
Alisema ikiwa mapendekezo hayo yatakubalika, maoni hayo yatawasilishwa kwenye kamati zote za Bunge hilo zinazoendelea kupitia na kujadili Rasimu ili yafanyiwe kazi.
MWANANCHI

No comments: