Hekalu la Freemasons lililopo katika Mtaa wa Sokine jijini Dar es Salaam. Picha na Rafael Lubava
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Sir Chande anasema kuwa, ingawa hakuiona ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza taarifa za Freemason Kenya, taasisi yake haikufanya jambo lolote baya.
Dar es Salaam. Wakati mwigizaji maarufu Stephen Kanumba alipofariki ghafla April 2012, aliacha mjadala na maswali kwa wapenzi wake, kama alikuwa mwanachama wa Freemason au la.
Tangu wakati huo, baadhi ya watu wamekuwa wakijitokeza hadharani na kueleza namna walivyoingizwa Freemason kwa lengo la kupata utajiri na nguvu.
Siyo hivyo tu, baadhi ya familia jijini Dar es Salaam zimejikuta mikononi mwa matapeli, baada ya kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ahadi ya kuingizwa kwenye Freemason ili kupata utajiri.
Mtanzania mmoja, ambaye alianzia ngazi ya chini hadi kufikia kuwa kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki, akiongoza zaidi ya vitengo 50, anaeleza kwa undani namna alivyojiunga na chama hicho akiwa bado kijana. Akiwa na umri wa miaka 24, Jayantilal Keshvji Chande, maarufu zaidi kwa jina la Sir Chande, alikuwa tayari ameshavutiwa kujiunga na Freemason, lakini hakujua vipi na wapi kwa kuanzia.
Kwa maneno yake, Sir Chande anasema kuwa hamu ya kujiunga na Freemason ilichochewa na tabia ya rafiki zake wawili wa wakati huo, Mwingereza, Bob Campbell Ritchie na John McLean kutoka Scotland.
Rafiki zake hao walikuwa na ratiba isiyokuwa ya kawaida hasa wakati wa jioni. Kila Jumatatu baada ya kutoka kazini, walikuwa wakihudhuria kile alichokiita ‘vikao vya kushangaza’ kwenye jengo moja lililopo karibu na bahari, Dar es Salaam.
Taratibu, udadisi wa Sir Chande kuhusu sehemu waliyokuwa wakienda rafiki zake ikajulikana, baada ya wao wenyewe kumweleza kuwa walikuwa ni wanachama wa Freemason.
‘Haraka nilitaka kuwa mwanachama’, anaandika Sir Chande katika kitabu chake “Usiku Afrika; Njia kutoka Bukene.” Kwa kuwa kujiunga Freemason siyo kwa kutuma maombi au kwa usaili, bali kwa kupendekezwa, haikuwepo njia nyingine ya kufanya hivyo.
Marafiki zake Sir Chande walimtambulisha kwa wanachama wa Freemason wengine, Sheikh Mustafa na Jivraj Patel, ambao kwa mwanzoni walilazimika kuwa kama ndugu yao kwa kuwa walikuwa wakifahamika ndani ya chama hicho.
Ilimchukua Sir Chande miaka miwili ya kusubiri, kuchunguzwa na kuona kama alikuwa na uadilifu unaohitajika kujiunga katika chama hicho, kinachodaiwa kujihusisha na giza na siri ikiwamo matambiko na kutoa kafara za binadamu kupata utajiri na nguvu.
“Kama ambavyo nilitarajia,” anaandika Sir Chande akieleza: “Nilitakiwa kusubiri kwa miaka miwili wakati naangaliwa kama ninaweza kufaa.”
“Hakuna mtu ambaye alinionya kuhusu maumivu anayoyapata mtu wakati wa kipindi cha matazamio, bila kujali masuala ya kifedha au msimamo wake kwenye jamii,” anaandika.
Kwa mujibu wa Sir Chande, wakati wa kuchunguzwa, kazi zake zote za kila siku, ndani na nje ya ofisi zilikuwa zikifuatiliwa kwa umakini mkubwa. Baadhi ya rafiki na ndugu zake pia walihojiwa.
“Ingawa nilikuwa natoka katika familia za watu wenye asili ya Asia waliofanikiwa kibiashara Afrika Mashariki, haikusaidia kurahisisha,” anaandika na kuongeza kuwa baada ya miaka miwili alijiunga na moja ya taasisi hatari duniani.
Kujiunga Freemason siyo kwa kuomba au kusailiwa tu. Kinyume na wengi wanavyodhani, badala yake kwa mujibu wa Sir Chande, mtu anakuwa mwanachama kwa kupendekezwa na mtu ambaye tayari ni mwanachama.
Tuhuma za kumwabudu shetani
Kama kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki, Sir Chande alikatishwa tamaa wakati taasisi yake ilipokuwa ikihusishwa na kumwabudu shetani na kutumia nguvu zisizo za kawaida za uchawi kama njia ya kushinikiza uamuzi nchini Kenya.
Mwaka 1994, karibu miaka minane tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Freemason Afrika Mashariki, aliitwa kufika mbele ya Rais Daniel Arap Moi wa Kenya kwenye uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoisakama taasisi hiyo.
“Kwa uelewa wangu, labda siyo kwa mshangao, niliitwa kufika mbele ya tume kwa nafasi yangu kama mkuu, kutoa ushahidi,” anaandika katika kitabu chake.
Ilisemekana kuwa Freemason walikuwa wakiliunga mkono kabila moja lililokuwa likiipinga Serikali na wanachama wake wakimwabudu shetani kwa kusali wakiwa uchi na kutoa kafara za binadamu kwa ajili ya kuchochea nguvu zao.
“Hii haikuwa mara ya kwanza,” anaandika Sir Chande akieleza kwamba pia zimekuwapo kashfa hata kwenye siasa kuhusu Freemason.
“Wachache wanaweza kusahau kashfa ya P2 nchini Italia, ambayo ilileta aibu na kuchafua taswira ya siasa kuhusu Freemason duniani kote,” anaandika.
Sir Chande anasema kuwa, ingawa hakuiona ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza taarifa za Freemason Kenya, taasisi yake haikufanya jambo lolote baya.
“Kwa kuwa tuhuma zilitolewa dhidi ya Freemason Kenya, ziligeuka kuwa baraka, ikatoa nafasi ya kufahamika zaidi katika umma na binafsi, ikizingatiwa kuwa kwenye Freemason siasa ni biashara yako binafsi kama ilivyo dini yako, wala siyo mambo ya majadiliano,” anaandika.
Hata hivyo, Sir Chande anaandika kuwa Tanzania haijawahi kukumbana na changamoto hizo kwenye siasa kutoka serikalini, hata wakati wa Azimio la Arusha kama ilivyotokea Uganda na Visiwa vya Shelisheli.
Kwa mujibu wa Sir Chande, hali hiyo ilitokana na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye wakati wa uhuru aliziangalia taasisi za kujitolea nchini na kuamini kuwa zote zilikuwa zikifanya kazi kwa mrengo wa kusaidia.
Je, Freemason ni taasisi yenye mambo yaliyofichika?
Kwa mujibu wa Sir Chande, Freemason ilianza baada ya Vita ya Pili ya Dunia (WW II), wakati udugu wa Kifreemason walipokuwa wakijaribu kuwalinda wanachama wao waliokuwa Ufaransa, Italia na Ujerumani dhidi ya mateso.
“Tangu wakati huo, tumeingia kwenye jamii na tumekuwa tukipuuza shutuma na kuwaonyesha kuwa taasisi yetu inamchukua mtu mzuri na kujaribu kumfanya kuwa mzuri zaidi, bahati mbaya siyo kila mtu amekuwa akikubaliana na suala hili.Sir Chande anaeleza: “Freemason ni maisha yanayotakiwa mtu ayaishi na siyo kuyafuatilia, ni maisha yaliyojikita kwenye dini, maadili, kulainishwa na ushirika mzuri, kupewa utu kupitia misaada na kujitolea kusaidia.Mafunzo ya Freemason siyo kwa ajili ya leo, bali ni milele. Ni nguvu ya kutenda mema na kuwa imara na inafundisha wanachama wake kuwa imara, kujiheshimu na kuwaheshimu wengine.
”Credit:Mwananchi
1 comment:
Cheo cha SIR (Knighthood)hutumiwa kwa jina moja tu la kwanza,usahihi ni Sir Andy na si vinginevyo.
Post a Comment