Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda
Na James Magai, Mwananchi
Yeye adai ni mzigo anaotwisha kutokana na kutetea kile alichokiita masilahi.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemtaka katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda aeleze sababu za kuwa na kesi nyingi, huku akihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu nchini.
Pia mahakama hiyo imeamuru vyombo vya dola kuacha kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani kusikiliza kesi zake, na kushauri kama wana wasiwasi nao, waweke mashine za ukaguzi katika mlango wa kuingilia mahakamani hapo.
Mwenendo huo wa Sheikh Ponda ulihojiwa mahakamani hapo na Jaji Augustine Shangwa juzi kabla ya kuanza kusikiliza rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai, mwaka 2012.
“Sheikh Ponda, sijui ni kwa nini una kesi nyingi kiasi hiki. Kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi (Kisutu) una kesi, Mahakama Kuu una kesi. Nani yuko nyuma ya kesi zako? Je! Serikali inakuchukia?” alihoji Jaji Shangwa.
Licha kumhoji Sheikh Ponda maswali hayo, alimweleza kuwa kama atakuwa na jambo la kuzungumza, atampa nafasi siku nyingine rufaa yake itakapotajwa. Pia Jaji Shangwa alimshauri apunguze mapambano.
“Ikiwezekana uyapunguze (mapambano) maana dunia hii si ya kupambana nayo,” alisema Jaji Shangwa na kusisitiza kuwa lazima ajiulize kwa nini ana kesi nyingi.
Jaji Shangwa aliendelea kusema: “Jambo likitokea Zanzibar, wewe umo; likitokea Morogoro umo; likitokea Dar es Salaam umo. Bahati mbaya kuna kikundi cha Uamsho kinadaiwa kulipua mabomu na kuua watu, nasikia na wewe unatajwa kuhusishwa.”
Hata hivyo baadaye Jaji Shangwa alimuuliza Ponda kama ana la kueleza kuhusu wingi wa kesi zinazomkabili.
Sheikh Ponda alidai kuwa kesi hizo ni mzigo anaotwisha kutokana na kutetea kile alichokiita masilahi, huku akijitetea kuhusu hukumu ya kesi iliyomtia hatiani ambayo amekata rufaa kuipinga, akieleza kuwa eneo analodai kuvamia ni mali ya Waislamu.
Hata hivyo, Jaji Shangwa alimkata kauli akisema anayoyaeleza yanapaswa kusemwa na mawakili wake katika rufaa hiyo kama alikuwa na hatia au la. Alimtaka aeleze ni kwanini anakabiliwa na kesi nyingi.
Hata hivyo, wakili wake Juma Nassoro alisimama na kuieleza Mahakama kuwa si kwamba mteja wake ana kesi nyingi, bali anakabiliwa na kesi mbili tu moja iliyokuwa Mahakama ya Kisutu ambayo ndiyo wameikatia rufaa na ile iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Awali, wakati akivipiga ‘stop’ vyombo vya dola kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani, Jaji Shangwa alisema: “Huyu Sheikh Ponda ana wafuasi wengi, wanahitaji kuja kusikiliza kesi yake. Vyombo husika visiwazuie, waacheni waje wasikilize kesi ya Sheikh wao.” Pia aliwaonya wafuasi hao kuacha mapambano na vyombo vya dola “Mnaweza kuona kama vile Sheikh wenu anasulubiwa lakini hapa hasulubiwi bali haya ni mashtaka ya kawaida tu ambayo anatakiwa kuyajibu,” alisema.
Kuhusu rufaa yake, Jaji Shangwa aliamua isikilizwe kwa njia ya maandishi na pande zote, mrufani (Ponda) na mjibu rufani (Jamhuri) watawasilisha hoja zao za rufaa na majibu ya hoja hizo kwa njia ya maandishi na kisha kusubiri hukumu.
Katika rufaa hiyo, Ponda anadai hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Katika kesi ya msingi, Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, na uchochezi.
Katika hukumu yake ya Mei 9, 2013, Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wa Mahakama ya Kisutu alimtia hatiani Ponda peke yake kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la Agritanza Ltd, lakini ikawaachia huru washtakiwa wengine wote.
Licha ya kumtia hatiani Ponda, mahakama hiyo ilimwachia huru kwa masharti ya kutotenda kosa lolote katika kipindi cha miezi 12.
Credit:Mwanachi
1 comment:
Ni mhalifu ,kwani wingi wa kesi si = wingi wa makosa?
Post a Comment