ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 23, 2014

Phiri kuwalea Simba kama baba

Kocha mpya wa Simba, Mzambia Patrick Phiri

Kocha mpya wa Simba, Mzambia Patrick Phiri amesema kuwa kwa soka la Afrika, walimu wanatakiwa kuishi na wachezaji kama watoto wao na ndivyo atakavyowalea wachezaji wa klabu hiyo.

Phiri alikuwa akizungumza na Nipashe ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa Simba umtimue kazi aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Mcroatia Zdravko Logarusic kwa tuhuma za kuwafokea na kutukana wachezaji wake wanapokosea.

Akizungumza na gazeti hili, Phiri ambaye amerejea Simba kwa mara ya pili kuifundisha timu hiyo kwa kipindi chake cha tatu alisema kazi inakuwa nyepesi endapo kunakuwa na uhusiano mzuri kati ya kocha na wachezaji wake.


“Kwangu mimi natambua umuhimu wa kuishi vizuri na wachezaji, nawafahamu wachezaji wa kiafrika," alisema kocha huyo aliyewahi kuifundisha timu ya taifa ya Zambia.

"Nilikuwa hapa Simba miaka ya nyuma na nimeishi vizuri na wachezaji na ndio maana kila ninaporudi wananipokea vizuri na wanaonyesha furaha yao mimi kuwepo hapa."

Kuwa karibu na wachezaji kunamfanya kocha kujua vizuri tabia za wachezaji wake za nje na ndani ya uwanja.
"Ukali usiokuwa na sababu si mzuri.

"Na si kila sehemu kocha unatakiwa kutumia ukali, si mzungumzii kocha aliyenitangulia bali ndiyo uhalisia kwa sababu hata kwenye familia zetu mambo kama haya yapo."

Phiri alisema amepania kurudisha ushindi na furaha kwa timu hiyo kama alivyofanya mwaka 2010/2011 ambapo aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Bara bila ya kufungwa hata mchezo mmoja.

Uongozi wa Simba chini ya Rais wake Evance Aveva ulimtimua Logarusic kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wachezaji kwamba ni mkali na mwenye kuwatukana.

Beki wa kati, Joseph Owino ni mmoja wa wachezaji ambaye amewahi kuingia kwenye mgogoro n a kocha huyo baada ya kutolewa lugha chafu.

Kwa sasa Phiri yupo na kikosi cha Simba visiwani Zanzibar ambapo kimeweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu iliyopangwa kuanza Septemba 20.

Katika mchezo wake wa kwanza, Simba itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa siku moja baadaye.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: