ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 11, 2014

SHUKURANI KUTOKA KWA RAIS WA JUMUIYA YA DMV


Kwanza kabisa napenda kuwashukuru wagombea wote kwa kushiriki kwenye uchaguzi wa Jumuiya ya watanzania hapa Washington DC, Maryland na Virginia.  Napenda kuwapongeza wagombea wote kwa kutimiza wajibu wao wa kidomokrasia na kushiriki kwa moyo mmoja na lengo moja ili kuweza kuijenga jumuiya yetu ya DMV.

Pia napenda niwashukuru watanzania wote mlioshiriki kwenye uchaguzi. Uchaguzi huu umeonyesha ni jinsi gani wana DMV tulivyo na muamko na jumuiya yetu na pia ni uthibitisho wa hali ya juu unaonyesha ni jinsi gani tunavyo thamini na kutekeleza haki yetu ya kidemokrasia. Nawaomba tuendelee kuitambua haki yetu  hii na tuendelee kuwa pamoja.

Pia napenda kuipongeza tume ya uchaguzi kwa kazi nzuri kwenye kulisimamia swala hili zima la kidemokrasia.  Pamoja na Tume napenda kuushukuru Ubalozi wetu kwa kuwepo kila walipohitajika au walipoona kuna haja ya kuchangia na kuhakikisha kuwa uchaguzi wetu unafanyika kidemokrasia.  Na vile vile napenda  nishukuru Montgomery County Police Force na Prestige Security  kwa ulinzi waliotupatia kwenye uchaguzi wetu.

Kwenda mbele mimi ni Rais wa Watanzania wote wa hapa DMV na ninawahakikishia kuwa nitashirikiana nanyi kwa moyo mmoja na nitaendelea kuwasikiliza ninyi wana DMV ili tuendelee kuipeleka Jumuiya yetu mbele. Jumuiya yetu inatuhitaji sisi sote,  niko tayari kushirikiana nanyi kuweza kuipeleka Jumuiya yetu mbele.

Nawaomba nyote tushirikiane kwa pamoja na tuendelee kuitangaza Junuiya yetu ya DMV, na tuendelee kuipepereusha bendera yetu ya Tanzania hapa USA na kuiletea nchi yetu sifa nzuri.

Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki ATC- DMV

Wenu 
Iddi Sandaly
Rais
Jumuiya Ya Watanzania DMV