ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 23, 2014

Walima matunda walilia kiwanda

Mchuuzi wa matango katika eneo la Chekereni Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro akitafuta wateja wa matunda hayo jana, ambapo alikuwa akiuza Sh1,000 kwa fungu moja lililopo kwenye bakuli. Picha na Dionis Nyato 
Na Salim Mohammed, Mwananchi
Ni kutokana na ahadi lukuki zilizotolewa na viongozi kushindwa kutekelezwa kwa wakati.
Pangani. Wakulima wa matunda na mbogamboga wilayani hapa, wameiomba Serikali itekeleze ahadi yake ya kuwajengea kiwanda cha kusindika matunda ili wajihakikishie soko la uhakika.
Wakizungumza katika Kongamano la Machungwa na Matunda lililofanyika juzi, wakulima hao walisema kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika, mazao yao huozea shambani na hivyo kujikuta wakiingia hasara kubwa.

Walisema hata wapatapo soko kutoka kwa wafanyabiashara wanaowafuata vijijini, hulazimika kuyauza kwa bei ya hasara.
“Sisi wakulima wa machungwa na mbogamboga tutazidi kuwa maskini na tutaendelea kuwatajirisha wenye fedha. Tukivuna machungwa tukakaa nayo ndani zaidi ya siku tatu au nne huoza, hivyo tunalazimika kuyauza kwa bei ya kutupa ili mradi tuambulie hata fedha kidogo,” alisema Jumanne Mhina, mkazi wa Mkwaja.

Hata hivyo, Wakulima hao walihoji tatizo linalokwamisha kujengwa kwa kiwanda hicho ambacho waliahidiwa muda mrefu na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Mwenyekiti wa wakulima wa machungwa, Fikirini Juma alisema tatizo hilo linawafanya kwa sasa waendeshe kilimo hicho kama sehemu ya bustani badala ya zao la biashara kutokana na kutokuwa na faida nalo.
Alisema mbali ya kukosekana kwa soko, pia barabara ni tatizo jingine linalochangia mazao yao kuharibika.

No comments: