ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 26, 2014

AFRIKA ISINYANYAPALIWE KWA SABABU YA EBOLA- JK



Na Mwandishi Maalum, New York
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na viongozi wengine duniani katika kuichagiza Jumuiya ya Kimataifa kuzisaidia Liberia, Siera Leone na Guinea mataifa ambayo yameathirika vibaya na mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola.

Amesema misaada inayopelewa na itakayopelewa katika nchi hizo inatakiwa kuwa endelevu na ya uhakika hadi pale ugonjwa huo utakapodhibitiwa,
Rais Kikwete ametoa wito huo siku ya alhamisi wakati alipokuwa akilihutubia Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa katika majadiliano ya jumla ( General Debate) yaliyoanza siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Akaongeza pia kwamba nchi za Afrika ya Magharibi na nyingine barani Afrika zinatakiwa kujengewa uwezo ukiwamo wa namna ya kuchunguza ugonjwa huo, kuwa na maeneo maalum ya wagonjwa pamoja na huduma za matibabu.

Kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika za kufanikisha upatikanaji wa tiba ya uhakika ya ugonjwa huo, tiba ambayo amesema itasaidia pia kuimarisha afya za wale ambao tayari wameathiria.

Akizungumzia zaidi kuhusu mlipuko wa Ebola na athari zake, Rais ametaka kuwapo kwa ushirikiano ndani ya jumuiya ya kimataifa hususani nchi zenye uwezo mkubwa wa kifedha na utaalam ili kwa umoja wao waweza kuwasaidia wanasayasi ambao wanaendelea na jitihada za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa wa Ebola.

Pamoja na kutaka mataifa yaliyoathirika na Ebola kusaidiwa kwa hali na mali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani ameitaka pia Jumuiya ya Kimataifa kutoinyanyapaa Afrika kwa sababu ya Ebola

Akasema taarifa za kuwapo kwa watu wanaofuta au kuahirisha safari zao za kwenda Afrika eti kwa sababu ya Ebola zinasikitisha

“Umoja wa Mataifa na Marafiki wa Afrika,saidieni kuwaeleza kwamba Afrika ni Bara lenye nchi 53.Afrika siyo nchi moja, Nchi nyingi ziko mbali sana na nchi nchi ambazo zimeathirika kwa Ebola. Na kwa kweli pengine nchi zilizoathirika ziko karibu zaidi na Ulaya kuliko mataifa mengine ya Afrika”

Akaongeza “Tusaidieni kupaza sauti ya Afrika ya kutonyanyapaliwa kwa sababu ya Ebola” akasema Rais. Kauli iliyopigiwa makofi na wajumbe waliokuwa wakimsikiliza.

Katika hotuba yake pamoja na kuuzungumzia kwa kina mlipuko wa Ebola, Rais Kikwete pia alizungumzia kuhusu maeneo mengine muhimu hususani katika Usalama wa Kimataifa, ambapo aligusia matukio ya kigaidi yanayoendeshwa na makundi kama Al Shaabab, ISIS na Boko Haram katika maeneo mbalimbali na kwamba makundi hayo hayapashwa kuachwa kuendelea na uovu wao.

Akayataja maeneo mengine ambayo yanaendelea kuifanya dunia kutokuwa mahali salama kuwa ni pamoja na mwendelezo wa uvunaji haramu wa mali asili, uwindaji haramu, biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha.

Aidha ametoa wito wa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu wa migogoro inayoendelea huko Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudani ya Kusini.

Kuhusu Palestina Rais amesema dunia haihitaji kusubiri zaidi hasa kutoka na mikasa ambayo imesababisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia wakiwamo watoto, wanawake na wanaume kupotea bila sababu.

Na kwa sababu hiyo ametoa wito wa Umoja wa Mataifa, Marekani, Urusi na Mataifa ya mengine ya Ulaya yafikie mahali pa kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro kati ya Palestine na Israel jambo alilosema kuwa linawezeka.

Kwa upande wa Sahara ya Magharibi ambalo ni koloni pekee barani Afrika, Rais Kikwete ameiutaka Umoja wa Mataifa na wadau wengine kulitafutia ufumbuzi ili nalo lifike tamati.

Rais pia alizungumza tatizo la muda mrefu la vikwzo vya kiuchumi ambavyo imewekewa Cuba, akazungumzia pia tatizo na changamoto ya mabadiliko ya Tabia nchi,na mchakato wa maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo endelevu ambayo alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na mataifa mengine katika eneo hilo.

No comments: