ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 9, 2014

Ajali nyingine mabasi zaua 8,kujeruhi 42

Watu nane wamefariki dunia na wengine 40 kujeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kupata ajali kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Kigoma, Morogoro na Tanga.

Kati ya watu hao, wanne walifariki katika ajali iliyotokea mkoani Morogoro, wawili Kigoma na wawili Tanga.

Aidha, kati ya waliojeruhiwa, 36 katika ajali iliyotokea mkoani Morogoro na sita Kigoma.

MOROGORO
Ajali ya Morogoro ilitokea baada ya basi la Kampuni ya Air Bus lililokuwa likitoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Tabora kutumbukia katika mto, uliopo katika Kijiji cha Kiegea njia panda ya kwenda Hospitali ya Berega, wilayani Morogoro.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11.45 katika barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kulihusisha basi hilo aina ya Scania lilokuwa likiendeshwa na Hilay Seif, mkazi wa jijini Dar es Salaam, ambaye inadaiwa baada ya ajali hiyo alikimbia.

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, ambaye alikutwa katika eneo la tukio, Joa Athuman, alisema walipofika katika kijiji hicho, basi hilo lilianza kuyumba na ndipo dereva aliwaambia usukani haufanyi kazi na kumtaka kila mmoja kuchukua tahadhari kisha yeye akarudi nyuma kukaa na abiria.

“Alituambia kuwa usukuni haufanyi kazi, hivyo kila mtu ajiandae kwa lolote. Na ndipo ghafla tukaanza kuporomoka katika daraja la mto huu mpaka chini. Ndiyo hali iliyotokea,” alidai abiria huyo.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kata Berega, James Minghhondwa, akizungumza katika eneo la tukio hilo, alisema basi hilo likiwa katika mwendo kasi, ghafla liliacha njia na kuteremka kwa kasi na kutumbukia mtoni.

Alisema kabla ya basi hilo kutumbukia mtoni, lilikuwa likiyumba katika barabara hiyo, hali iliyoashiria lilikuwa limepata hitilafu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, vifo hivo na majeruhi hao, wakiwamo wanaume 18, wanawake 10 na watoto sita.

Alisema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Berega kwa matibabu na kwamba, maiti ambao hawajatambuliwa wanahifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kusuburi ndugu kujitokeza kuwachukua kwa ajili ya maziko.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Berega, Dk. Afred Chiponda, alithibitisha kupokea majeruhi 34, kati yao, saba hali zao ni mbaya, ambao wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.

KIGOMA
Ajali ya Kigoma ilitokea katika Kijiji cha Kanyonza, Wilaya ya Kakonko, mkoani humo Kigoma, jana majira ya saa 5.00 asubuhi, ikihusisha basi la Kampuni ya Mohamed Trans lenye namba za usajili T273ACX aina Scania.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Toima Kiroya, alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Karimu Sulemani likitokea Kigoma kwenda Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Alisema lilipofika katika kijiji hicho, liliacha njia na kuanguka na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwamo mwanamke, ambaye hajatambulika na mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja na kwamba, miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko.

Kiroya alisema majeruhiwa sita, ambao ni Masanja Wandure (48), ambaye alipata jeraha kichwani, Pendo John (18) aliyechubuka mgongoni na mikononi, Berania Venasi (40) aliumia mguu wa kulia, Eshiboni Bakina (15) aliyepata michubuko mwilini, Edisa Masunzu (30) aliyeumia kichwani, Careful Yusufu (5) aliyeumia mgongoni, wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba, kutokana na eneo hilo kuwa na kona kubwa, dereva alishindwa kulimudu basi hilo, hivyo likapoteza mwelekeo na kukatika ‘henga’ ya mbele na kuanguka.

Kiroya alisema dereva wa basi hilo, Karimu Sulemani, alikimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya ajali hiyo. Basi hilo lilikuwa limebeba abiria 50.

DC aliwataka madereva wawe makini katika uwendeshaji wa magari ili kuepuka ajali hasa magari ya abiria kwa kuzingatia sharia za barabarani kwa sababu hali za barabara za mkoani hapo ni za vumbi nyingi wakati wa kiangazi.

Aidha alisema madereva wawe waangalifu katika kupishana kwa sababu barabara hiyo ni nyembamba pia ni ya vumbi.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kigoma Jafari Mohamed alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa Jeshi hilo linamshikilia Tingo wa basi hilo ambaye hajatambulika jina lake na uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.

KOROGWE
Ajali ya Tanga ilitokea baada ya gari dogo aina ya Toyota Verosa lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro kuacha njia na kutumbukia mto Mkomazi Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi mkoa huo, Abdi Isango, alisema ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu ya Mombo Hedaru eneo la Mbuta lililopo kijiji cha Mkomazi Mombo.

Isango aliwataja waliokufa katika ajali hjiyo kuwa ni dereva wa gari hilo, Kipaa Alex Mbowe (42), na abiria wake, Pili Richard na Neemia Gwao (36), mfanyabiashara mkazi wa Mbezi jijini Dar. .

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na ulevi.Alisema polisi walipofanya uchunguzi ndani ya gari hilo walikuta kuna chupa za bia aina ya Serengeti.

Nayo mabasi ya Kampuni ya Simba Mtoto na Dar Express yamegongana uso kwa uso katika barabara kuu ya Dar kwenda Arusha.Abiria zaidi ya 100 waliokuwa wakisafiri kwenye mabasi hayo walinusurika.

PWANI
Wakati huo huo, askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kituo cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Koplo E7133 John Masele (44), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kuachia njia na kupinduka katika Kijiji cha Masaki, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.

Gari hilo lenye namba za usajili T582AKG Pajero, lilipata ajali baada ya gurudumu lake la mbele kupasuka.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Athuman Mwambalaswa, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 9, mwaka huu, majira ya saa 9.00 usiku.

Alisema Masele aliumia kichwa na kufariki hapo hapo na kwamba, mwili wake ulipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchnguzi zaidi.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kanda Maalumu Dar es Salaam, Camillius Wambura, alimzungumzia marehemu Masele akisema alikuwa ni mchapakazi na mwenye upendo.

Alisema Jeshi la Polisi limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na askari aliyekuwa akifanya kazi bila ya kukumbushwa na mwenye upendo kwa kila mmoja.

Kamanda Wambura alisema baada ya kupata taarifa za ajali hiyo, alishikwa na butwaa kutokana na kuondokewa na askari mchapakazi na alikuwa anafanya kazi bila ya kusimamiwa.

“Kwa kweli watu huwa wanasema mtu akifa ndio anarundikiwa sifa, kwa hili sikubaliani nalo, nasema toka moyoni, Masele alikuwa ni mchapa kazi na alikuwa ni mtu mwenye upendo kwa kila mtu,’’alisema.

Alisema wiki iliyopita, marehemu alihitimu mafunzo ya ukakamavu na kwamba,mwili wake uliagwa katika Kanisa la AIC Magomeni na ulitarajiwa kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Wilaya ya Bunda, mkoani Mara kwa maziko.

Imeandikwa na Joctan Ngelly (Kigoma), Ashton Balaigwa (Kilosa), Yasmine Protace (Pwani) na Steven William (Muheza).
CHANZO: NIPASHE

No comments: