Advertisements

Wednesday, September 10, 2014

Bomu lamkata mtoto vidole tisa

Arusha. Mtoto Lowassa Kivuyo (14), amelazwa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center, baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu na kumkata vidole tisa vya mikono yake.

Akizungumza kwa tabu katika hospitali hiyo, mtoto huyo alisema tukio hilo lilitokea Jumapili Septemba 7, mwaka huu saa tisa mchana akiwa na wenzake watatu walipokuwa wakichunga ng’ombe.

Alisema waliona kitu kama kifuniko cha mpira ambacho kilikuwa kimefungwa na kuanza kurushiana na wenzake, Charles Ngine, Baraka Silonga na Long’otuti Petro na ghafla kililipuka.

Alisema mwenzake, Petro alijeruhiwa kichwani huku ng’ombe watatu pia wakijeruhiwa na kitu hicho.

Kaka wa Lowassa, ambaye anamtunza hospitalini hapo, Maige Kivuyo alisema tukio hilo lilitokea eneo la Elperera, Kata ya Sepeko wilayani Monduli.

“Alikuwa na wenzake wanachezea kwa kurushiana kitu ambacho tunadhani ni bomu na ndipo kililipuka,” alisema.`

Kivuyo alisema eneo hilo ni la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lakini huwa wanaruhusiwa kuingiza mifugo yao mara baada ya mazoezi kumalizika.

Muuguzi wa zamu wa wodi namba mbili, kitengo cha mifupa, alipolazwa Lowassa, Deodata Mahela alisema mtoto huyo amekatika vidole tisa na amebaki na kimoja cha mkono wa kushoto.

“Hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu, kwani pia alikuwa amepata majeraha mengine kidogo pembeni ya kifua,” alisema Mahela.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema jeshi halina taarifa za tukio hilo.

“Tutachunguza mara moja na kupata ukweli wa taarifa hiyo,” alisema.

Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Pole sana waliojeruhiwa....ningeshauri muendelee fuatilia na muelimishwe ili tukio kama hilo lisiwakumbe watu wa jamii yenu.
kila la kheri.