ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 28, 2014

MICHEZO YA SHIMIWI YAFUNGULIWA RASMI

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Celina O. Kombani (Mb) akifungua mashindano ya michezo ya SHIMIWI mjini Dodoma leo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw.Noeli Kazimoto akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo ya SHIMIWI mjini Dodoma leo.
Watumishi wa Serikali kutoka Wizara na Idara za Serikali wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Celina O. Kombani (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI mjini Morogoro leo.
Watumishi wa Serikali kutoka Wizara na Idara za Serikali wakiwa kwenye maandamano kabla ya ufunguzi wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI mjini Morogoro leo.
Meza kuu ikipokea maandamano kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo ya SHIMIWI mjini Morogoro.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Celina O. Kombani akisalimiana na wageni waalikwa na viongozi mbalimbali wa serikali alipowasili kwenye viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro kwa ajili ya ufunguzi wa michezo ya SHIMIWI.
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI wakisalimiana na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Celina O. Kombanimjini Morogoro leo.

Na Happiness Shayo

Waajiri katika Wizara,Idara Zinazojitegemea,Wakala na Taasisi za Serikali wametakiwa kuhakikisha kuwa wanaweka bajeti ya kutosha na utaratibu mzuri wa michezo kwa watumishi wao ili kujenga ukakamavu,afya na pia kufahamiana.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Celina O. Kombani (Mb) alisema hayo leo alipokuwa akifungua mashindano ya SHIMIWI mjini Morogoro.

“Pamoja na changamoto za ufinyu wa bajeti na kuwa na kazi nyingi,waajiri wanatakiwa wadumishe michezo sehemu za kazi”alisema Mh.Kombani

Mh.Kombani alifafanua kuwa pamoja na mambo mengine michezo inaepusha maradhi ya mara kwa mara hasa yanayosababishwa na uzito uliokithiri.

Aidha,Mh.Kombani aliwataka wanamichezo kuwa na mshikamano na kushirikiana katika kipindi chote cha michezo.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw.Noeli Kazimoto aliwataka wanamichezo wanaoshiriki SHIMIWI wazingatie maadili ya Utumishi wa Umma hata kama wako nje ya vituo vyao vya kazi.

“Lazima tuzingatie maadili na kudumisha nidhamu tunapoendelea na michezo hii kwa kuwa sisi bado ni watumishi wa Umma”alisema Bw.Kazimoto.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mashindano hayo, Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw.Danieli Mwalusamba alitoa shukrani kwa uongozi wa mkoa wa Morogoro kwa kutoa ushirikiano wa kutosha hadi kufanikisha mashindano hayo.

Wakati huohuo, timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Timu ya mpira wa miguu ya Mkoa wa Arusha zilitoka bila kufungana baada ya mechi za ufunguzi kuanza huku timu ya netiboli ya Ikulu ikishinda kwa kete 62 dhidi ya timu ya Mkoa wa Morogoro iliyoambulia kete 10.

Kwa upande wa timu za kamba, timu ya wanaume ya Ikulu iliibuka mshindi kwa pointi 2 baada ya kuiburuza timu ya kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa huku timu ya kamba wa wanawake ya Wizara ya Uchukuzi ikiibuka kidedea baada ya kuivuta timu ya kamba ya wanawake ya Mkoa wa Iringa na kushinda kwa pointi 1.

Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) huandaa mashindano yanayowakutanisha watumishi wa Serikali kila mwaka lengo kuu ikiwa ni kuendeleza tabia ya ushirikiano, upendo na undugu.

No comments: