Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema uamuzi wake wa kuitetea Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na tume aliyoiongoza, pamoja na kauli yake ya juzi ya; ‘Tutakutana mtaani’, havimaanishi kwamba atakihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jaji Warioba amesema jana kwamba baada ya kutoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), baadhi ya watu wakiwamo makada wa CCM wanaodhani kuwa atajiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika maandamano ya kudai Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.
Katika kongamano hilo, Jaji Warioba alisema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba Septemba 24 mwaka huu bungeni mjini Dodoma, imeondoa mambo manne muhimu na mengine mengi yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.
Akizungumza na gazeti hili Jaji Warioba alisema: “Juzi (jana) niliposema kuwa tutakutana mtaani, nilikuwa namaanisha kwamba tutakutana na Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika midahalo, makongamano, semina na katika vyombo vya habari. Sisi tutaendelea kuitetea rasimu tuliyoitoa Desemba mwaka jana. Wao (wajumbe wa Bunge la Katiba), tutakutana nao huko huko ili wawaeleze wananchi sababu za kuondoa maoni yao.”
Jaji Warioba aliyeiongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa miezi 20 ikiratibu na kukusanya maoni ya wananchi na mabaraza ya katiba ngazi mbalimbali, alisema kuwa kamwe hawezi kujiunga na Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na DP kwa sababu vyama vya siasa viliuteka mchakato huo na kuuharibu.
“Ieleweke kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inasimamia katika maoni ya wananchi na haiwezi kuyumba katika hilo. Tutaendelea kusisitiza kuheshimiwa kwa maoni hayo na wale waliyoyabadilisha, lazima wawaeleze wananchi sababu za kufanya hivyo,” alisema.
Aliongeza: “Inashangaza kuona watu wakihusisha kauli yangu ya juzi na kujiunga na Ukawa au vyama vya siasa. Tusubiri tu, ikifika wakati wa kupiga kura ya maoni ili tuone wananchi watakubali rasimu ipi.”
Katika ufafanuzi wake, Jaji Warioba alisema kuwa hata suala la mgombea huru limewekwa masharti mengi yanayoweza kuwa kikwazo kwa mgombea.
“Mgombea huru kawekewa masharti ambayo binafsi naona kama ni ya kumkataa kistaarabu. Suala la muungano nalo pia ni tatizo na bado halijapatiwa ufumbuzi,” alisema.
MWANANCHI
1 comment:
Jaji Warioba! Wewe upo kwenye upande mzuri wa history
Post a Comment