Advertisements

Tuesday, September 2, 2014

MISINGI YA USAWA WA JINSIA IKILINDWA KATIKA KATIBA MPYA, TUTAPATA KATIBA YENYE MRENGO WA JINSIA

Baadhi ya Wajumbe wanawake wa Bunge Maalum la Katiba wakiimba kwa furaha wakati wa semina iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba (wa kwanza kulia) akipitia taarifa ya mapendekezo ya mtandao wa wanawake na Katiba Tanzania wakati wa semina iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya akitoa mada kuhusiana na suala la kijinsia katika Katiba, wakati wa Semina iliyoandaliwa na Umoja huo kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwaajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya Jinsia na Katiba iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa Mjini Dodoma.

Usawa wa jinsia ni hali ya wanawake na wanaume kuwa na fursa sawa na upatikanaji wa haki zenye kuleta tija katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ya jamii.Kati ya makundi haya mawili, lengo kuu la kuwepo kwa usawa wa jinsia ni kuhakikisha kuwa raia wote wanapewa nafasi ya kukua na kuondolewa vikwazo mbalimbali ili waweze kuchangia na kutambuliwa kwa usawa katika maendeleo yao ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi pamoja na kisiasa.

Ili Katiba iwe yenye mrengo wa jinsia hainabudi iwe inayotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake na wanaume wakati wa uandaaji wake na pia iliyoweka bayana makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza nchi ikibeba sauti zao.

Sambamba na hilo, Katiba hainabudi kuzingatia misingi ya demokrasia ikiwemo utawala wa sheria wenye kuwajibika kwa wananchi, usawa wa jinsia, utu na heshima ya kibinadamu kwa kila raia wakiwemo wanawake na wanaume, watoto wa kike na wa kiume.Aidha, Katiba iwe inayowezesha uwepo wa misingi mikuu ya usawa kati ya wanaume na wanawake katika vipengele mbalimbali vya Katiba.

Bila shaka twapaswa kujua kuwa Katiba ni‘Sheria Mama’ inayolinda haki za raia wote wakiwemo wanawake, wanaume na watoto nchini na kuainisha mfumo wa kuendesha nchi na wajibu wa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza. Hivyo,ni vema Sheria hii Mama iwe imebeba masuala ama haki za makundi haya mbalimbali nchini kwa kudumisha maendeleo yenye tija.

Usawa wa jinsia ni msingi muhimu kwenye maendeleo ya nchi yeyote ikiwemo nchi yetu Tanzania, ambapo tafiti mbalimbali za hapa nchini na kwingineko zinaonyesha kuwa kwenye sekta ambazo zinatekeleza mipango yenye kulenga katika kukidhi mahitaji ya wanawake na wanaume pamoja na kutambua michango yao mbalimbali zimeleta tija zaidi kimaendeleo.

Ujenzi wa misingi ya usawa wa jinsia kwenye Katiba Mpya ni muhimu kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo ya Afrika na Ulimwenguni ambayo imesaini Mikataba mingi ya Kimataifa na Kikanda ya kutekeleza Katiba, sera, sheria na mipango iliyojengewa kwenye misingi ya usawa wa jinsia nchini.

Mikataba hii inajumuisha Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto, Mpango wa Utekelezaji wa Mikakati ya Beijing, Protokali ya Makubaliano ya Haki za Binadamu na Usawa wa Jinsia ya Umoja wa Afrikapamoja na mikataba mingine kadha wa kadha.

Hivi karibuni, tumeona ama kusikia juu ya Semina iliyofanywa Bungeni mjini Dodoma na Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba wakijadili juu ya umuhimu wa uwepo wa masuala ya jinsia katika Katiba Mpya na masuala muhimu ya jinsia ya kuzingatiwa katika katiba, ambapo wabunge hao waliweka mkazo katika suala zima la haki sawa katika Katiba kati ya wanawake na wanaume yani Hamsini kwa Hamsini.

Wabunge wanawake wa Tanzania wakishirikiana kwa pamoja na Mtandao wa Wanawake na Katiba waliweka bayana madai ya haki zao katika Katiba Mpyana madai haya ni kama ifuatavyo;-
Haki za wanawake zibainishwe kwenye Katiba Mpya, Sheria kandamizi zibatilishwe, Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na umiliki rasilimali ya nchi,

Utu wa mwanamke ulindwe, Utekelezwaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu haki za wanawake, Haki sawa katika nafasi za uongozi, Haki za Wanawake wenye ulemavu, Haki ya uzazi salama, Haki za watoto wa kike, Haki ya kufikia na kufaidi huduma za msingi, Wajibu wa wazazi katika matunzo ya watoto pamoja na Katiba iunde chombo maalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kimsingi, madai haya yote ya haki sawa yanayodaiwa na Wabunge hawa yana umuhimu mkubwa katika Katiba Mpya itakayopatikana kwani ndiyo yatayopelekea kupatikana kwa Katiba yenye mrengo wa jinsia.

Akitoa mada wakati wa semina hiyo, Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya alisema kuwa suala la msingi wa usawa wa jinsia ni muhimu kuwekwa katika Katiba Mpya na baadaye kuwepo na uwajibikaji wake kwani kwa kufanya hivyo kutaipatia nchi katiba yenye mrengo wa kijinsia.

Bi. Mallya aliongeza kuwa wanawake wengi nchini wamekuwa hawapati fursa ya usawa wajinsia katika nyanja mbalimbali licha ya Tanzania kuwa kinara wa kutoa wanawake vinara ambao wamewahi kushika nyazifa mbalimbali na wengine bado wakiendelea kushika nafasi hizo za juu hapa nchini.

“Utafiti unaonyesha kuwa, asilimia 5% ya wanawake nchini ndiyo wanaomiliki ardhi, asilimia 39% ya wanawake hao hao hawapati elimu ya kutosha, pia utafiti unaonyesha kuwa asilimia 40.3% ya wanawake walioko kwenye ajira wapo katika sekta isiyo rasmi, wakati asilimia 10% ya Maprofesa wanawake ndiyo tunayo hapa nchini”, alisema Bi. Mallya.

Aidha, Bi. Mallya alizitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake wengi nchini kuhusiana na usawa wa jinsia na haki zao pamoja na haki za watoto huku akitoa taarifa za utafiti zinazoonyesha kuwa mzigo wa kazi wa asilimia 66% ya wanawake wanafanya kazi zisizo na kipato, na asilimia 44% ya wanawake nchini walioolewa katika ndoa zao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.

Naye Mwenyekiti wa Women Fund Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba, Profesa Ruth Meena alizungumzia juu ya masuala ya umuhimu wa jinsia ya kuzingatiwa katika Katiba Mpya huku akisisitiza juu ya usawa wa uongozi katika ngazi zote uwe hamsini kwa hamsini na uwepo wa chombo maalum kitakachozingatia haki za wanawake.

Profesa Meena alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa Katiba Mpya iweze kulinda haki za watoto kwa kutoruhusu ndoa za utotoni, hivyo kuwepo na sheria zitakazo mlinda mtoto dhidi ya ndoa hizo mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka (18) Kumi na nane.

“Suala la umri wa mtoto wa kike kuolewa iwe ni miaka Kumi na nane, na mtu atakayeoa mtoto chini ya miaka kumi na nane awe amebaka”,alishauri Profesa Meena.

Aidha, Profesa Meena aligusia kuhusu masuala ya haki ya uzazi salama kwa wanawake pindi wanapojifungua, liweze kupewa kipaumbele kwa kujali usalama wa maisha ya mama na mtoto na isiwe hukumu ya kifo kwa akina mama.

“Iwe ni haki yetu ya uhai tunapofanya kazi ya kuongeza kizazi cha Tanzania, wanawake wapewe usalama wa uzazi wanapozaa pasipokuwa na kigugumizi, hivyo kuzaa kusiwe hukumu ya kifo kwa watoto wetu”,alisema Profesa Meena.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia alihudhuria katika semina hiyo, aliwatia moyo Wabunge wanawake hao na kuwataka kuwa na umoja wa kudai haki zao za usawa wa jinsia na alisisitiza juu uwepo wa ushirikiano kati ya wanaume na wanawake katika jamii.

Mhe. Samia hapa anawataka wanaume kuwaunga mkono wanawake kwa kuwapa nafasi za uongozi na waepuke tabia ya kuwadharau wanawake katika masuala mbalimbali yakiwemo uongozi ama kuwapa talaka kutokana kuwa na hofu, pindi wanawake wapatapo fursa ya uongozi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba naye ameitaka jamii kuwekea mkazo suala la elimu ya uzazi, kuwa ianze kutolewa kuanzia elimu ya msingi ili watoto waweze kuwa na uelewa wa kutosha pindi wanapokuwa wakubwa, Aidha alitoa hamsini kwa hamsini katika masuala yote katika jamii.

Kwaupande wawajumbe wengine wa Bunge hilo, Mhe. Hamad Rashid aliwashauri wanawake kuacha kutegemea Viti Maalum kwenye nafasi za ubunge kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga uwezo na kujiamini kuwa wanaweza.

“Mnapopata nafasi za uongozi mzitumie vizuri ili kuweza kujiamini na kujituma,” alisisitiza Mhe. Hamad. NayeWaziri Rajabu Salum mjumbe wa Bunge hilo, alisisitiza juu ya umuhimu wa elimu kuhusu masuala ya kijinsia yatolewe kwa msuguano, kwani wanaume wengi hawana uelewa wa jambo
hilo.

Agatha Senyagwa ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo, kutoka kundi la 201 upande wa wakulima, alisema ni vema elimu juu ya masuala ya kijinsia kwa wanawake wa vijijini ili nao wawe na uelewa kwa ajili ya kushiriki katika kugombea nafasihususan ngazi ya Serikali za Mitaa, mfano uwenyekiti wa kijiji na watendaji kata.

Ili kufanikisha uwepo wa Katiba hii yenye mrengo wa jinsia, hatunabudi kuingiza haki mahsusi (Gender specific) za wanawake na watoto wa kike katika Katiba, pia kuingiza misingi imara ya usawa wa jinsia na ile inayolinda haki za wanawake (Gender equality outcomes) katika vipengele mbalimbali vya Katiba.

(Picha zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma).

No comments: