Advertisements

Saturday, September 13, 2014

Ugonjwa mpya waingia nchini

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt. Seif Rashid
Geita. Hatimaye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa matokeo ya sampuli zilizopelekwa Nairobi nchini Kenya, kubaini chanzo cha utata wa kifo cha Bertha Boniphace (25) aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Geita, mkoani hapa baada ya kuenea uvumi kuwa alikuwa akiumwa ugonjwa wa ebola.
Akizungumza kuhusu matokeo ya sampuli hizo jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk Adam Sijaona alisema matokeo kutoka Nairobi yanaonyesha Bertha hakuwa na ugonjwa wa ebola bali alikuwa anaumwa ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Chikungunya Viral Hemorrhagic Fever (VHF).
“Matokeo yametoka rasmi hakuuawa na ugonjwa wa ebola kama tulivyozungumza awali ila unaelekea kwenye kundi la ebola, dengue na homa ya bonde la ufa. Ni ugonjwa wa kitropiki. Kitaalamu tunauita Arthropod borne virus, unaenezwa na mbu aina ya Aedes Aegyti,” alisema Dk Sijaona na kuongeza:
“Aina hii ya mbu ni wachache na wanapatikana kwenye maeneo yenye unyevuvyevu kama wengine, Bertha alikuwa akifanya kazi maeneo ya madini Kata ya Katoro ambako mbu hao ni rahisi kupatikana.
“Lakini siyo ugonjwa wa kawaida nchini ingawa siyo hatari kama virusi vya ebola. Ni kesi chache za aina hii kwa sababu tangu apatikane huyu hadi leo hakuna mgonjwa mwingine aliyeripotiwa, ila watu wanatakiwa kuchukua tahadhari.”
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Joseph Kisala alisema ugonjwa huo ni mpya nchini na kwamba, haujazoeleka barani Afrika na kama ilivyo kwa magonjwa ya VHF hauna tiba maalumu.
Dalili zake
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), aina ya magonjwa ya VHF yana tabia ya homa za mara kwa mara, mwili kudhoofika, kutokwa na vipele vidovidogo mwili mzima, kutokwa damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani na masikioni na kwamba dalili hizo ni kama za dengue.
Bertha Boniphace (25) alifariki dunia Agosti mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, huku kifo chake kikisababisha uvumi kuwa alikuwa anaumwa ebola hatua iliyosababisha uongozi wa mkoa kukanusha uvumi huo.
Mgonjwa huyo alitokea Kata ya Karoro-Buserere akisumbuliwa na kutapika, kuharisha damu na kutoka damu sehemu za mdomo na puani, dalili ambazo zinashabihiana na zile za ugonjwa wa Ebola hali iliyosababisha watu kufikiria kuwa ameuawa na ugonjwa huo.
Kutokana na utata huo, uongozi wa hospitali ulichukua tahadhari muhimu kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo huku ukikataa kutoa mwili kwa ndugu zake kwenda kuuzika na kuchukua jukumu la mazishi hayo.
MWANANCHI

No comments: