Advertisements

Friday, October 17, 2014

Majeruhi wa moto wazidi kupoteza maisha Dar

Lori mali ya Kampuni ya Moil Transporter lililokuwa likisafirisha mafuta ya petroli kwenda Kampala, Uganda lilipinduka likiwa na lita 38,000 na kisha kuwaka moto.

Dar es Salaam. Majeruhi wa moto uliotokana na mlipuko wa lori la mafuta huko Mbagala Rangi Tatu, Dar es Salaam wameendelea kupoteza maisha baada ya wengine wawili kufariki dunia na kufanya idadi yao kufikia saba.
Lori mali ya Kampuni ya Moil Transporter lililokuwa likisafirisha mafuta ya petroli kwenda Kampala, Uganda lilipinduka likiwa na lita 38,000 na kisha kuwaka moto.
Ofisa Habari Msaidizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dorice Ishenda alisema waliofariki dunia hadi kufikia jana asubuhi ni Nurdin Mazinga (24) na Abbas Uganga (21) hivyo kufanya waliofariki dunia kufikia saba na majeruhi wengine tisa wakiendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo.
“Hata hivyo, majeruhi saba wanaopata matibabu hali zao ni mbaya sana na wanahitaji uangalizi wa karibu zaidi. Madaktari wameendelea kutafuta namna za kitaalamu zaidi kuokoa maisha yao kutokana na majeraha makubwa ya moto waliyoyapata,” alisema.
Alisema majeruhi wawili tu kati ya tisa, ambao hali zao angalau zinatia matumaini kutokana na kuweza kuzungumza na kutokuwa na majeraha makubwa ya kutisha.
Wengine waliopoteza maisha awali ni Mohamed Hassan (36), Hassan Ismail (19), Maulid Rajab (61) na Mohamed Ismail (21).
Idadi hiyo inafanya watu waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo kufikia saba, akiwamo wa kwanza aliyefariki kwenye tukio hilo kabla ya kufikishwa hospitali.
Chanzo cha ajali
Chanzo cha ajali hiyo ni watu waliokuwa wakichota petroli iliyomwagika baada ya lori hilo kupinduka. Wachotaji hao walificha mafuta hayo kwenye nyumba za jirani na mlipuko huo ulipotokea moto ulifuata mafuta hayo na kuleta madhara kwenye eneo hilo.
Juzi Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Amani Malima alisema walikuwa wamebaki majeruhi wanne.
Mwananchi

No comments: