
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Omari Nundu
Alisema halmashauri zimeshindwa kutimiza ahadi ambazo serikali imezitoa kwa wananchi kutokana na watumishi kukosa uaminifu.
Nundu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Uchukuzi, aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tangamano mjini hapa ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Alisema, Tanga ya leo siyo ya miaka ya nyuma kutokana na kukumbwa na changamoto kubwa.
"Jiji la Tanga limekosa watumishi waaminifu, ndiyo wanaofanya lisipige hatua kutokana na watumishi hasa wa halmashauri kutofanya kazi ipasavyo," alisema Kinana.
Alisema kuwa, serikali katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa na maisha bora ilitenga fedha nyingi kupitia halmashauri kwa ajili ya kutoa fursa kwa akina mama na vijana, lakini fedha hizo hazikuwafikia.
Alifafanua kuwa, sheria ya kutengwa kwa fedha kwa ajili ya makundi hayo ilipitishwa mwaka 1993 na kwamba vijana wanatakiwa kupewa asilimia tano na akina mama asilimia tano lakini katika halmashauri hiyo hakuna kinachofanyika.
"Pamoja na halmashauri kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha makundi hayo lakini bado mimi na mke wangu tulijibana na kuamua kutoa fedha sehemu ya mshahara wangu na kupata fedha zaidi ya Sh.milioni 10, kwa lengo la kuwakopesha wananchi wangu, niliowakopesha nao wameshindwa kurejesha fedha hizo ninadai zaidi ya Sh.milioni 3."alisema Nundu.
Alisema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/15 katika jimbo kwa sehemu kubwa ameweza kutatua kero mbalimbali za wananchi wake.
Aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada zake za kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Akizungumzia Bandari ya Tanga Nundu alisema kuwa wakati akiwa waziri wa uchukuzi aliikuta bandari hiyo ikiwa na hasara ya Shilingi bilioni mbili lakini alifanya jitihada za kuhakikisha bandari hiyo inajiendesha kwa faida.
Hata hivyo, Mbunge huyo alimsifu Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, kuwa anafanya kazi kubwa ya kuimarisha chama hicho kwani kazi anayofanya kila mtu anaiona na kuna kila sababu ya kuunga mkono kazi kazi zake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment